
Mwl Nyerere wenzio wanavunja Muungano
Na DANIEL MBEGA
Salaam Mwalimu Nyerere,
Sina shaka kwamba huko uliko umepumzika kwa amani, kwa uwezo wa
Mungu. Yawezekana umekuwa mwenyeji huko na kazi yako njema uliyoifanya
katika kuhakikisha Tanganyika inajitawala, na hatimaye inaungana na
Jamhuri ya Watu wa Zanzibar kuzaa Tanzania, bado ni kitambulisho tosha
ndiyo maana leo hii, miaka 14 baada ya kifo chako, bado Watanzania
tunakukumbuka huku duniani.
Lakini nina uhakika hujui yanayotokea huku Tanzania. Kwa kifupi,
mambo yameharibika. Natamani waraka wangu ungekufikia mwenyewe mkononi
ili nikukumbushe ama nikupashe yanayoendelea huku.
Wale wote uliowanadi mwaka 1995 ili waienzi Ikulu yetu, walikugeuka
miezi michache tu baada ya wewe kulala na babu zako. Wakaigeuza Ikulu
kuwa sehemu ya biashara – ingawa wapo wengine uliwauliza “…Mnakimbilia
Ikulu kufanya biashara gani!” Viwanda vyote ulivyopigania kuanzishwa
waauziana wenyewe. Ikulu ikawa sehemu ya kusaini mikataba mibovu ambayo
immeshuhudia madini yetu yalikuvunwa na kupelekwa nje huku sisi tukibaki
na mashimo tu.
Kwa kifupi, uliona wanafaa walikusailiti. Maadili ya uongozi
uliyoyasisitiza yakatoweka. Vita ya rushwa imeshindikana kwani wenye
dhamana ya kupambana nayo ndio vinara wa kutoa na kupokea rushwa.
Natamani hata Chifu Fundikira angekuwepo naye aone wenzake wanavyofaidi –
pengine angesikitika kwa nini yeye aliondolewa kwenye Baraza lako la
Mawaziri miaka michache tu baada ya uhuru.
Ufisadi umetamalaki kila kona, chaguzi zimegubikwa na rushwa mbaya.
Chama chako cha Mapinduzi kimekuwa ‘Chama cha Matajiri’. Bora hili ni
neon zuri, lakini wengine wanakiita ‘Chama cha Mafisadi’, au ‘Chama cha
Majangili’ na wengine wanathubutu kusema ni ‘Chama cha Majambazi’,
ilimradi kila mmoja anatamka neno analoona linafaa. Maskini hawana
nafasi, wachache tu ndio wana sauti kwa sababu ya fedha zao.
Wale uliowapinga ndani ya Chama wakati ule, uliowahoji kuhusu
walikopata utajiri wao, leo hii ndio wanaoabudiwa. Mbaya zaidi wanapita
mpaka misikitini na makanisani kutoa misaada, halafu wanapigiwa makofi
na kuimbiwa mapambio. Ungewaona, nina imani ungemwaga machozi. Naamini
mama yetu Maria anaugulia moyoni kwa yanayotokea.
Mwalimu, sikuwepo wakati huo, lakini nakumbuka ilikuwa Jumapili,
Aprili 26, 1964, saa 4.00 asubuhi wakati wewe – ukiwa Mwenyekiti wa TANU
– ulipokutana na Mwenyekiti wa Afro-Shiraz Party (ASP) Sheikh Abeid
Amani Karume mjini Dar es Salaam na kusaini hati ya makubaliano ya
kuziunganisha nchi zenu. Muungano huu ulifikiriwa kwa takribani miezi
mitatu na siku 24 tu tangu yalipofanyika mapinduzi ya kuung’oa utawala
dhalimu wa Kisultani visiwani Zanzibar Januari 12, 1964. Kabla ya kutiwa
saini, nyote wawili mlikuwa mmefanya mazungumzo mara kadhaa mjini Dar
es Salaam na Unguja na ndipo mkafikia mwafaka wa kuziunganisha nchi
hizo.
Wapo walioupinga wakati huo (na wanaendelea kuupinga) kwamba
haukufuata misingi inayotakiwa katika muungano halisi, lakini pia wapo
walioufurahia na wanaendelea kuufurahia kwa kuwa umeleta udugu na
kujenga umoja na mshikamano.
Mwalimu, imebaki miezi michache tu ili Muungano huu utimize miaka
50, lakini nina mashaka kama hautakufa kabla ya miaka hiyo kutimia.
Umoja, amani, upendo na mshikamano uliojengwa na muungano huo umetoweka
kabisa.
No comments:
Post a Comment