ADVERT 1

ADVERT 1
Kilio na kimbilio la wanahabari Tanzania

Sunday, November 17, 2013

MAMIA WAJITOKEZA KUAGA MWILI WA DKT MVUNGI ,MAKAMU WA RAIS DKT BILAL AWAONGOZA WATANZANIA

Makamu wa Rais Dk. Mohammed Gharib Bilal akitoa salamu za Rais Jakaya Kikwete wakati wa  Ibada  ya kuuaga   mwili  wa aliyekuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba  marehemu  Dk. Sengodo Mvungi  kwenye viwanja vya Karimjee leo jijini Dares Salaam.

Makamu wa Rais Dk. Mohammed Gharib Bilal akitoa heshima za mwisho kwa  mwili  wa aliyekuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba  marehemu  Dk. Sengodo Mvungi  kwenye viwanja vya Karimjee leo jijini Dares Salaam.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akitoa heshima za mwisho kwa  mwili  wa aliyekuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba  marehemu Edmond Sengodo Mvungi  kwenye viwanja vya Karimjee leo jijini Dares Salaam.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad akitoa heshima za mwisho kwa  mwili  wa aliyekuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba  marehemu  Dk. Sengodo Mvungi  kwenye viwanja vya Karimjee leo jijini Dares Salaam

Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji mstaafu Joseph Warioba akitoa heshima za mwisho kwa  mwili  wa aliyekuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba  marehemu Dk.  Sengodo Mvungi  kwenye viwanja vya Karimjee leo jijini Dares Salaam.

Waziri Mkuu Mstaafu Cleopa Msuya akitoa heshima za mwisho kwa  mwili  wa aliyekuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba  marehemu Dk.  Sengodo Mvungi  kwenye viwanja vya Karimjee leo jijini Dares Salaam .


Rais Mstaafu wa  Serikali ya Awamu ya tatu Benjamin Mkapa  akitoa heshima za mwisho kwa  mwili  wa aliyekuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba  marehemu Dk. Sengodo Mvungi  kwenye viwanja vya Karimjee leo jijini Dares Salaam.



Mwenyekiti wa  Chama cha Wananchi(CUF)Profesa Ibrahim  Lipumba   akitoa heshima za mwisho kwa  mwili  wa aliyekuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba  marehemu Dk.  Sengodo Mvungi  kwenye viwanja vya Karimjee leo jijini Dares Salaam.


Mwenyekiti wa  Chama cha  NCCR -Mageuzi  James Mbatia     akitoa heshima za mwisho kwa  mwili  wa aliyekuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba  marehemu Dk.  Sengodo Mvungi  kwenye viwanja vya Karimjee leo jijini Dares Salaam.






Mwenyekiti wa Kambi ya Upinzani Bungeni,Freeman Mbowe akitoa heshima za mwisho kwa  mwili  wa aliyekuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba  marehemu Dk.  Sengodo Mvungi  kwenye viwanja vya Karimjee leo jijini Dares Salaam.
Watoto wa marehemu Dk.  Sengodo Mvungi  aliyekuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Natujwo (kushoto) na  Neema (kulia)  wakinadi shairi lakuelezea baba yao alivyojasiri  heshima kwenye viwanja vya Karimjee leo jijini Dares Salaam.
Mke wa marehemu Dk.  Sengodo Mvungi , Anna Mvungi (katikati)  akiwa katika ibada hiyo kwenye viwanja vya Karimjee leo jijini Dares Salaam

Msajili wa Vyama vya Siasa Jaji,Francis  Mutungi akizungumza katika msiba huo .
Waziri wa Habari ,Vijana , Michezo na  Utamaduni  Dk. Fenella  Mukangara  akiuaga  mwili.

Profesa Palamagamba Kabudi ambaye ni rafiki wa aliyekuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba  marehemu Dk.  Sengodo Mvungi  akitoa heshima kwenye viwanja vya Karimjee leo jijini Dares Salaam.

  Monsinyori Deogratius Mbiku (wa pili kulia ) akiongoza ibada na wenzake .


Familia ikiwa katika msiba.

Dk. Salim Ahmed Salim  akiaga mwili huo . (Picha  Fullshangwe blog na Magreth Kinabo)

Babu wa Loliondo atangaza watu kumiminika upya, Apata maono mengine.

millard
Millard Ayo wa Clouds FM Alipokua akifanya mahojiano na Mchungaji Ambilikile Masapila maarufu kama Babu wa Loliondo
Hivi karibuni mtangazaji maarufu Millard Ayo katika kipindi chake cha Ampifaya alifanya mahojiano na Mchungaji Ambilikile Masapila na kuelezea kwa urefu mwanzo wa huduma yake ya kikombe, changamoto, walioiga kutoa vikombe, vipingamizi pamoja na waliokufa, ambao hawakupona hawakufuata masharti ya dawa.
Mwishoni mwa mahojiano Babu wa Loliando akasema kuhusu mafuriko mapya yatakayotokea hivi karibuni huko Samunge, alizungumza hivi
Siwezi kusema moja kwa moja kwamba ni mwezi wa tatu, ingekuwa pengine mpaka sasa tungeanza kupata watu wengi, na inawezekana ikawa mwezi huo wa tatu, au kabla au baada, mimi siwezi kusema moja kwa moja kwasababu kuna vipingamizi vingi tu, ambavyo Mungu anasubiri vitimie ndipo kazi hiyo ianze, Kuna miujiza mingi imeandikwa ndani ya biblia kitabu cha Mwanzo, Zaburi, Ezekiel, Ufunuo yapo maajabu mengi ambayo Mungu ameyaandika hayakutimia katika nchi ya Israel yatatimia hapa, Samunge, kwahiyo mafuriko ya watu watakaokuja si kwa ajili ya kunywa dawa tu lakini ni kwa ajili ya mambo mbali mbali kuja kuona miujiza ya Mungu itakayofanyika
Alipoulizwa ni maajabu gani yatakayofanyika akasema
“Si vizuri, sijamwambia mtu yeyote ba hata hapa kwako sitasema, isipokuwa mimi nimeyaona mengi tu nimeyaona tayari lakini Mungu hajaniambia tangaza napewa (Maono) kila wakati linakuja hili, linakuja hili napewa kila wakati lakini si zaidi ya labda nusu mwaka sasa
Ili kulinganisha habari ndipo mtangazaji Millard Ayo alipomuuliza Mchungaji Onesmo Ndegi ni maajabu gani hayo ya kwenye biblia
Mchungaji akasema “Hakuna muujiza ambao haujatendeka zaidi ya ule muujiza wa unyakuo, miujiza mingine yote iliyotabiliwa ilishatendeka kwa mfano ukisoma muujiza mkubwa sana ambao Mungu aliuzungumza kutoka Mwanzo 3:15 biblia inasema hivi nami nitaweka uadui kati yako na huyu mwanamke na kati ya uzao wako na uzao wake huo utakuponda kichwa na wewe utauponda kisigino, sasa hapa alikuwa anazungumzia juu ya ujio wa Kristo na ushindi wa Kristo dhidi ya nguvu za giza au shetani na ilishatokea na tunaishi katika kipindi hicho, Yesu Kristo alishakuja akazaliwa, na uwezo wake ukadhibitika ushindi dhidi ya shetani ulionekana pale msalabani, kwa hiyo hakuna muujiza mwingine ambao utasema kuanzia mwanzo haujatimia sasa kuna mtu anataka kuutimiliza, hakuna muujiza wa namna hiyo
Babu wa Loliondo alipoulizwa tena ana ushauri gani kwa Serikali juu ya maajabu  hayo makubwa yatakayotokea hivi karibuni akajibu
Nilitaka kusema kwa upande wa Serikali, nitasema ya kwamba Serikali iwe makini kupokea watu watakaokuja maana ni wengi, ni mafuriko kwa hiyo wawe makini”
Hata hivyo babu amewasamehe watu wote waliomsema vibaya “Kisasi ni kwa Bwana” alisema
–Millard Ayo

Ibada ya Kukabidhiana Msalaba wakati wa Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, Jimbo kuu la Dar es Salaam

Na: Kizito Ugulumo

Katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, Msalaba unachukua maana ya pekee katika maisha ya waamini, kwani wanatumwa na kuchangamotishwa kuwa ni mashahidi amini wa Kristo na Kanisa lake: kwa maneno na matendo. Msalaba ni kielelezo cha mapendo, neema, sala, msamaha na matumaini yasiyodanganya kamwe!

Ndiyo maana, Kanisa linaona fahari juu ya Msalaba wa Kristo kwa kuutembeza katika nyumba za waamini, ili wapate nafasi ya kusali na kulitafakari Fumbo la Msalaba, ishala ya mateso na alama ya wokovu wa binadamu; mahali ambapo hekima ya Mungu imetundikwa juu yake! Ni mwaliko wa kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu. Ifuatayo ni Ibada ya kukabidhiana Msalaba katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, Jimbo kuu la Dar es Salaam.

Vikundi vya pande zote mbili: wanaokabdhi na waokabidhiwa wanasimama mbele ya Msalaba. Padri wa kikundi kinachokabidhi msalaba anaanza ibada:

Padri: Kwa jina la Baba, na la Mwana, na la Roho Mtakatifu...
Wote: Amina.
Padri: Bwana awe nanyi..
Wote: Na awe rohoni mwako.

Padri anaeleza madhumuni ya kukutana:

Padri: Ndugu zangu, tumekutana hapa ili kukabidhiana Msalaba wa Mwaka wa Imani, ambacho ni chombo alichotumia Bwana wetu Yesu Kristo kutukomboa. Tunafanya tendo hili la ibada ya kuuheshimu Msalaba ili Mungu azidi kutujalia neema ambazo Kristo alitustahilisha kwa mateso, kifo na ufufuko wake. Tunawakabidhi Msalaba huu ili muupokee kama kumpokea Kristo mwenyewe katika parokia yenu. Uwe ishara ya ujio wake Kristo katika Mwaka huu wa Imani. Wakati wote utakaokuwa parokiani kwenu utunzwe na kuheshimiwa kama chombo kitakatifu kilicholeta wokovu. Ishara ya Msalaba huu iwaletee wingi wa neema za Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu.
Wote: Amina.

Sasa tusikilize somo linalotueleza kuwa Yesu Kristo ni Mwokozi wa ulimwengu:

Somo: Yohane (3:14-21)

Inafuatia tafakari fupi

Sala za Waamini:

Padri wa kikundi kinachopokea Msalaba anaongoza Sala za Waamini:

Padri: Ndugu zangu, Yesu Kristo amemtolea Mungu Baba maisha yake Msalabani ili ampatanishe na wanadamu. Ee Baba wa huruma uyasikie maombi yetu...
Wote: Bwana utuongezee imani

    Msalaba utukumbushe mapendo makubwa ya Kristo; Msalaba uamshe shukrani mioyoni mwetu...
    Msalaba uwe bendera ya Wakristo na alama ya ushindi wao; Msalaba ututie nguvu katika mateso, vitisho na hatari...
    Msalaba utufanye tuwe imara katika imani yetu, uwe nguvu yetu ya kuwafukuza pepo wabaya na washawishi...
    Msalaba uwe nguvu yetu ya kututoa katika dhambi na mazingira ya dhambi, ili sisi sote tuweza kuingia katika ufalme wa Mungu...
    Kwa ishara ya Msalaba tuwabariki wana familia zetu; tufanye ishara ya Msalaba maishani na kifoni...

Ee Mungu, umeweka Msalaba uwe ishara ya ukombozi wetu na alama ya huruma na mapendo yako. Twakuomba utupe neema ya kuuchukua Msalaba wetu pamoja na Mkombozi kwa mapendo makubwa. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
Wote: Amina.

Wanakabidhiana Msalaba Mtakatifu, huku ukiimbwa wimbo ufaao...

Wednesday, November 13, 2013





Je waijua bendera ya Tanganyika iliyokuwa ikipepea kabla ya Uhuru!

 



















Hiii ndiyo bendera ya Tanganyika ambayo kimsingi yapaswa kupepea tena baada ya kuundwa kwa serikali tatu.






 Na hii ndo bendera ya ndugu zetu itakayokuwa nchi jirani endapo muundo wa serikali tatu uliomo katika rasimu ya katiba utapitishwa




 Na endapo yote hayo hapo juu yasipotokea basi tutaendelea kupepea na bendera hii ambayo mpaka sasa ndo utambulisho wetu baada ya kuunganisha bendera hizo kuu za nchi mbili yaani Tanganyika na Zanzibar.



JE WAJUA MKWAWA ALIVYOWATEKETEZA WAJERUMANI KWA DAKIKA 15 TU!!!



HUU ni mfululizo wa Makala ya Uchunguzi kuhusiana na historia ya kiongozi mkuu wa Wahehe, Chifu Mkwavinyika Munyigumba Kilonge Mwamuyinga, maarufu kama Mkwawa, kama yanavyoandikwa na Mwandishi Wetu, ambaye amefanya uchunguzi kwa takriban miezi mitatu sasa katika kuhimiza utalii wa ndani na kuhifadhi historia yetu. Endelea na Sehemu hii 

HADI wakati huo, tayari von Heydebreck – mmoja wa manusura katika vita hivyo – alikuwa amekwishajeruhiwa na kuanguka akiwa amepoteza fahamu, lakini baadaye aliandika kwenye ripoti yake
“…Mfululizo wa matukio hadi wakati huu ulikuwa umetumia dakika mbili au tatu tu. Nilitambua hilo kabla ya kujeruhiwa, Wasudani tayari walikuwa wamekimbia kurudi nyuma vichakani baada ya kufyatua risasi mara mbili hivi. Mimi na askari wa Kikosi cha Tano tulilazimika kujilinda na kujitetea baada ya kuona Wahehe wakija katika umbali wa hatua 30. Kama sikosei, nilimsikia Sajini Tiedemann akisema alikuwa ameumia kabla hajafyatua risasi. Haikuwa rahisi kuona zaidi ya umbali wa hatua tano msituni kutoka pale njiani. Pia hakuna ambaye aliweza kunusurika kwa sababu Wahehe walikuja kwa kasi… Ni wazi walipanga kutushambulia baada ya kufika katikati msitu. Kuvurugika kwa mipango yao kulichangiwa hasa na kitendo cha Luteni von Zitewitz kufyatua risasi…”
Muanzilishi wa Himaya ya Ujerumani Afrika Mashariki, Carl Peters, baadaye Novemba 23, 1891 alimwandikia Gavana von Soden akisema kwamba, katika mapambano mengine na makabila mbalimbali ya Tanganyika, ilikuwa ni bahati tu kwao kutoweza kupata madhara kama waliyopata Wajerumani pale Lugalo, kwani mafunzo yao ya vita yalikuwa yanalenga zaidi kupigana wakiwa wamejipanga pamoja kwa mbinu maalum. Hawakuwa wamejifunza kupigana kila mtu kwa uwezo wake, bali walitegemea zaidi kushambulia kwa pamoja.
Iliwachukua Wahehe dakika 15 tu (kuanzia saa 1:15 hadi 1:30 asubuhi) kuwafyeka Wajerumani na majeshi yao. Von Zelewiski aliuawa kwa kupigwa nyundo kichwani akiwa amepanda punda wake wakati akijiandaa kuwafyatulia risasi wapiganaji wa Mkwawa. Kabla hajadondoka akachomwa mkuki ubavuni.
Hii ndiyo asili hasa ya jina la ‘Nyundo’ kutokana na kamanda huyo wa Wajerumani kuuawa kwa nyundo!
Kuhusiana na kifo cha Kamanda von Zelewiski, kama Mjerumani Tom von Prince alivyoandika baadaye, “Kama nilivyosimuliwa baadaye… na Wahehe walioshuhudia, alijitetea mwenyewe kwa kutumia bastola yake kubwa na kuwapiga risasi watu watatu, wakati kijana mmoja wa Kkihehe alipomchoma na mkuki ubavuni. Kijana huyo alikuwa na umri wa miaka 16 tu na alizawadiwa ng’ombe watatu na Mkwawa kwa kitendo hicho.”
Luteni von Pirch na Dk. Buschow pia waliuawa wakiwa juu wa punda wao ambapo majeraha yao yalikuwa makubwa mno. Karibu askari wote wa Kikosi cha 7, Kikosi cha Silaha, Kikosi cha 5 na baadhi ya askari wa Kikosi cha 6 waliuawa kabla hata hawajajua wafanye nini.
Luteni von Heydebreck, Luteni Usu Wutzer na Murgan Effendi pamoja na askari 20 hivi ndio waliofanikiwa kukimbia kutoka eneo hilo la mapigano na kukimbilia upande mwingine wa mlima na kuweka ngome wakijilinda dhidi ya mashambulizi ya Wahehe. Wapiganaji hao wa wajerumani walijificha kwenye pagala moja la tembe lililokuwa limetelekezwa mlimani. Askari mmoja Msudani ndiye aliyekiona kibanda hicho.
Lakini von Heydebreck aliishuhudia vita hiyo katika kipindi cha dakika mbili au tatu tu kabla ya kupoteza fahamu. “Kulingana na ushuhuda wa Wahehe walioshiriki mapigano yale, vita hivyo havikumalizika mapema kama ambavyo Wazungu wa mstari wa nyuma walivyotegemea, badala yake askari walionusurika waliendelea kupambana hadi saa 4:30 asubuhi na kuwaua maadui wengi (Wahehe).”
Askari wa mwisho wa kikosi cha Luteni von Tettenborn ndio hawakupata madhara makubwa ya mashambulizi ya Wahehe, washukuru kutokana na makosa ya ishara, vinginevyo wote wangeangamia katika kipindi hicho cha dakika 15 tu. Von Tettenborn, Feldwebel Kay na askari kama 20 hivi Wasudani wakahamia upande wa kushoto wa eneo la mapigano na kutengeneza nusu duara kwa ajili ya mashambulizi huku wakiwa wameumia. Wakiwa hapo walipandisha bendera ya Ujerumani juu ya mti na kupiga mbinja ili kuwaita manusura wengine.
Wakati huo Wahehe waliendelea kuwakimbiza manusura na kushambulia kila waliyemuona mbele yao. Mkanganyiko ukaongezeka baada ya kuwasha nyasi.
Mnamo saa 2:30 asubuhi hiyo, Luteni von Heydebreck, Luteni Usu Wutzer na Murgan Effendi wakiwa na askari wao 12 walipenya na kuungana na kikosi cha von Tettenborn. Von Heydebreck alikuwa anavuja sana damu kutokana na majeraha mawili makubwa ya mikuki. Kwa kuwatazama tu watu hao, von Tettenborn akatambua kwamba vikosi vyao vyote vilikuwa vimesambaratishwa na kikosi cha silaha kutekwa, ambapo Mkwawa aliteka bunduki 300. Askari wa jeshi la Wajerumani waliouawa siku hiyo walikuwa zaidi ya 500.
Ilipofika saa 3:00 Luteni Usu Thiedemann, akiwa na majeraha makubwa ya moto aliingizwa kwenye kikosi cha Luteni von Tettenborn akiwa amebebwa na askari waliokuwa wanafanya doria. Nyasi zilizokuwa zinaungua sasa zilimtisha von Tettenborn na manusura wengine.
Hadi kufikia saa 10:00 jioni Luteni von Tettenborn alikuwa amewakusanya majeruhi wengi na kuokota baadhi ya mizigo yao. Wahehe waliokuwa wamepagawa kwa hasira pamoja na moto mkubwa uliokuwa ukiendelea kuteketeza msitu viliifanya kazi ya kuwatafuta majeruhi wengine kuwa ngumu, hivyo wengi waliteketea kwa moto. Von Tettenborn akaamua kuanza kurudi nyuma kabla hajazuiwa na Wahehe.
Wakati wa usiku wa manane kikosi kilichokuwa na Luteni von Tettenborn kikapiga kambi ng’ambo ya pili ya mto tofauti na mahali walipolala kabla ya kuanza mapambano. Kikosi chake sasa kilikuwa na yeye mwenyewe na Luteni von Heydebreck, ma-NCO watatu wa Kijerumani (ingawa Luteni Usu Thiedemann alikufa baadaye njiani), maofisa wawili wa Kiafrika, ma-NCO 62 wa Kiafrika, wapagazi 74 na punda 7. Kutoka hapo wakaanza kutembea hasa nyakati za usiku kurudi nyuma ambapo walifika Myombo Agosti 29.
Hakuna takwimu halisi za idadi ya Wahehe waliokufa kwenye vita hiyo ingawa makadirio ni kati ya 260 hadi 700. Kwa ujumla, Wajerumani walikuwa wameshinda vita dhidi ya wakoloni, ushindi ambao ni wa kihistoria kwa mtawala yeyote wa Kiafrika wakati huo dhidi ya Wazungu. Haya yalikuwa matokeo mabaya zaidi kwenye vita katika historia ya ukoloni wa Wajerumani.
Jeshi la Wahehe halikuwa na haja ya kuhitimisha ushindi wake kwa kuwafuatilia Wajerumani waliosalia ili kuwaangamiza kabisa. Badala yake, kuanzia wakati huo wakaendelea kuishambulia misafara yote ya Wazungu.

MWILI WA DKT. SENGONDO MVUNGI KUWASILI IJUMAA NOVEMBA 15 2013, KINANA AMLILIA 

 

 Rais Jakaya Kikwete akitia saini kitabu cha maombelezo ya kifo cha Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Dkt. Sengondo Mvungi nyumbani kwake Kibamba jijini Dar es Salaam.
  Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Joseph Warioba wakifurahia jambo na Waziri wa Katiba na Sheria Mathias Chikawe (kushoto), Makamu Mwenyekiti wa Tume Jaji Mkuu Mstaafu Augustino Ramadhani na Mjumbe wa Tume Waziri Mkuu Mstaafu Dkt. Salim Ahmed Salim (kulia) walipokutana nyumbani kwa marehemu Dkt. Sengondo Mvungi Kibamba jijini Dar es Salaam.
(Picha na Tume ya Katiba)
  Rais Jakaya Kikwete (katikati) akibadilishana mawazo na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Joseph Warioba (kushoto) nyumbani kwa marehemu Dkt. Sengondo Mvungi walipokwenda kuipa pole familia. Kulia ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi James Mbatia na Mjumbe wa Tume Waziri Mkuu Mstaafu Dkt. Salim Ahmed Salim.
 Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Richard Lyimo akimpa pole mke wa marehemu Dkt. Sengondo Mvungi, Bi. Anna Mvungi wakati Wajumbe wa Tume walipokwenda kumpa pole.
  Rais Jakaya Kikwete akimpa pole mke wa marehemu Dkt. Sengondo Mvungi, Bi. Anna Mvungi alipokwenda kumpa pole nyumbani kwake Kibamba jijini Dar es Salaam.
 wenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Joseph Warioba wakifurahia jambo na Waziri wa Katiba na Sheria Mathias Chikawe (kushoto), Makamu Mwenyekiti wa Tume Jaji Mkuu Mstaafu Augustino Ramadhani na Mjumbe wa Tume Waziri Mkuu Mstaafu Dkt. Salim Ahmed Salim (kulia) walipokutana nyumbani kwa marehemu Dkt. Sengondo Mvungi Kibamba jijini Dar es Salaam.
(Picha na Tume ya Katiba)
.............................................................................................................................
Tume ya Mabadiliko ya Katiba inawafahamisha wananchi kuwa taratibu za kuusafirisha mwili wa Mjumbe wake, Dkt. Sengondo Mvungi aliyefariki nchini Afrika Kusini zimekamilika na mwili wake unatarajia kuwasili nchini siku ya Ijumaa, Novemba 15, 2013.

Baada ya kuwasili, mwili huo utahifadhiwa katika Hospitali ya Jeshi Lugalo iliyopo jijini Dar es Salaam.

Aidha, siku ya Jumamosi, Novemba 16, 2013 kutafanyika Ibada ya mazishi katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph jijini Dar es Salaam kuanzia saa 4:00 asubuhi. Baada ya misa, marehemu ataagwa katika Viwanja vya Karimjee kuanzia saa 6:30 mchana siku hiyohiyo ya Jumamosi, Novemba 16, 2013.

Aidha, Marehemu Dkt. Mvungi anatarajiwa kusafirishwa siku ya Jumapili, Novemba 17, 2013 kwenda Kisangara Juu, Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya mazishi yanayotarajiwa kufanyika siku ya Jumatatu, Novemba 18, 2013.

Dkt. Mvungi alifariki jana (Jumanne, Novemba 12, 2013) katika Hospitali ya Millpark jijini Johannesburg nchini Afrika Kusini alikopelekwa kwa ajili ya uchunguzi na matibabu zaidi akitokea Kitengo cha Mifupa Muhimbili (MOI) aliokuwa amelazwa baada ya kuvamiwa nyumbani kwake Kibamba, wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam na watu waliomjeruhi vibaya kichwani usiku wa kuamkia siku ya Jumapili, Novemba 3, 2013.

Wakati huohuo, Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba wakiongozwa na Mwenyekiti wake Jaji Joseph Warioba leo (Jumatano, Novemba 13, 2013) wameungana na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kufika nyumbani kwa marehemu Dkt. Mvungi eneo la Kibamba jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kutoa pole kwa familia, ndugu na jamaa wa marehemu Dkt. Mvungi.
Mwisho.
Imetolewa na:
Ndg. Assaa A. Rashid,
Katibu,
Tume ya Mabadiliko ya Katiba,
Dar es Salaam

 
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ndugu Abdulrahaman Kinana amesikitishwa na taarifa ya kifo Cha Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Dr Sengondo Mvungi kilichotokea Jana katika Hospitali ya Millpark nchini Afrika ya Kusini.

Kwa niaba ya Chama Cha Mapinduzi, Katibu Mkuu anawapa pole wanafamilia, Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Warioba na Uongozi wa Chama Cha NCCR-Mageuzi. Hakika Taifa limepoteza Mtaalamu wa Sheria, Kiongozi Mzalendo na hodari katika kipindi ambacho mawazo yake yanahitajika kwa kiasi kikubwa kuliendeleza Taifa hili.
Mwenyezi Mungu aiweke roho ya marehemu mahali pema peponi.
Imetolewa na:
KATIBU WA HALMASHAURI KUU YA TAIFA
ITIKADI NA UENEZI
13/11/2013
 
Habari kwa hisani ya www.francisgodwin.blogspot.com
Mwalimu Nyerere na Sheikh Karume

 Mwl Nyerere wenzio wanavunja Muungano


Na DANIEL MBEGA
Salaam Mwalimu Nyerere,
Sina shaka kwamba huko uliko umepumzika kwa amani, kwa uwezo wa Mungu. Yawezekana umekuwa mwenyeji huko na kazi yako njema uliyoifanya katika kuhakikisha Tanganyika inajitawala, na hatimaye inaungana na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar kuzaa Tanzania, bado ni kitambulisho tosha ndiyo maana leo hii, miaka 14 baada ya kifo chako, bado Watanzania tunakukumbuka huku duniani.
Lakini nina uhakika hujui yanayotokea huku Tanzania. Kwa kifupi, mambo yameharibika. Natamani waraka wangu ungekufikia mwenyewe mkononi ili nikukumbushe ama nikupashe yanayoendelea huku.
Wale wote uliowanadi mwaka 1995 ili waienzi Ikulu yetu, walikugeuka miezi michache tu baada ya wewe kulala na babu zako. Wakaigeuza Ikulu kuwa sehemu ya biashara – ingawa wapo wengine uliwauliza “…Mnakimbilia Ikulu kufanya biashara gani!” Viwanda vyote ulivyopigania kuanzishwa waauziana wenyewe. Ikulu ikawa sehemu ya kusaini mikataba mibovu ambayo immeshuhudia madini yetu yalikuvunwa na kupelekwa nje huku sisi tukibaki na mashimo tu.
Kwa kifupi, uliona wanafaa walikusailiti. Maadili ya uongozi uliyoyasisitiza yakatoweka. Vita ya rushwa imeshindikana kwani wenye dhamana ya kupambana nayo ndio vinara wa kutoa na kupokea rushwa. Natamani hata Chifu Fundikira angekuwepo naye aone wenzake wanavyofaidi – pengine angesikitika kwa nini yeye aliondolewa kwenye Baraza lako la Mawaziri miaka michache tu baada ya uhuru.
Ufisadi umetamalaki kila kona, chaguzi zimegubikwa na rushwa mbaya. Chama chako cha Mapinduzi kimekuwa ‘Chama cha Matajiri’. Bora hili ni neon zuri, lakini wengine wanakiita ‘Chama cha Mafisadi’, au ‘Chama cha Majangili’ na wengine wanathubutu kusema ni ‘Chama cha Majambazi’, ilimradi kila mmoja anatamka neno analoona linafaa. Maskini hawana nafasi, wachache tu ndio wana sauti kwa sababu ya fedha zao.
Wale uliowapinga ndani ya Chama wakati ule, uliowahoji kuhusu walikopata utajiri wao, leo hii ndio wanaoabudiwa. Mbaya zaidi wanapita mpaka misikitini na makanisani kutoa misaada, halafu wanapigiwa makofi na kuimbiwa mapambio. Ungewaona, nina imani ungemwaga machozi. Naamini mama yetu Maria anaugulia moyoni kwa yanayotokea.
Mwalimu, sikuwepo wakati huo, lakini nakumbuka ilikuwa Jumapili, Aprili 26, 1964, saa 4.00 asubuhi wakati wewe – ukiwa Mwenyekiti wa TANU – ulipokutana na Mwenyekiti wa Afro-Shiraz Party (ASP) Sheikh Abeid Amani Karume mjini Dar es Salaam na kusaini hati ya makubaliano ya kuziunganisha nchi zenu. Muungano huu ulifikiriwa kwa takribani miezi mitatu na siku 24 tu tangu yalipofanyika mapinduzi ya kuung’oa utawala dhalimu wa Kisultani visiwani Zanzibar Januari 12, 1964. Kabla ya kutiwa saini, nyote wawili mlikuwa mmefanya mazungumzo mara kadhaa mjini Dar es Salaam na Unguja na ndipo mkafikia mwafaka wa kuziunganisha nchi hizo.
Wapo walioupinga wakati huo (na wanaendelea kuupinga) kwamba haukufuata misingi inayotakiwa katika muungano halisi, lakini pia wapo walioufurahia na wanaendelea kuufurahia kwa kuwa umeleta udugu na kujenga umoja na mshikamano.
Mwalimu, imebaki miezi michache tu ili Muungano huu utimize miaka 50, lakini nina mashaka kama hautakufa kabla ya miaka hiyo kutimia. Umoja, amani, upendo na mshikamano uliojengwa na muungano huo umetoweka kabisa.

Mpiganaji wa ukweli na kiongozi wa kabila dogo la wahehe aliyetikisa Ujerumani




Hili ni kaburi la Mtwa Munyigumba Kilonge Mdegella Mwamuyinga lililo katika Kijiji cha Rungemba wilayani Mufindi, takribani kilometa 61 kutoka Iringa mjini.

Na Daniel Mbega
MAANDIKO kadhaa yamekuwepo kuhusiana na historia ya Wahehe na hasa ukoo wa Mtwa Mkwavinyika Munyigumba Mwamuyinga, maarufu kama Mkwawa, lakini yote hayo hayakunizuia kuisaka historia hiyo.
‘Jicho halishibi kuona na Sikio halikinai kusikia!’ hivyo nikaamua kufunga safari hadi Lungemba, yaliko makaburi ya Mtwa Munyigumba na ndugu wengine wa ukoo huo, yapata kilometa 62 kutoka Iringa Mjini.
Wapo walioandika kwamba chimbuko la Mtwa Mkwawa ni Ungazija, lakini simulizi ninazokutana nazo hapa ni tofauti, maana zinatoka katika vinywa vya wanaukoo wa Muyinga, ambao nao wameipata ama kurithishwa kutoka kizazi na kizazi kutokana na simulizi za mababu zao.
Wale waliopata kuandika kwamba asili ya akina Mkwawa ni Ungazija wanaeleza kuwa mtawala wa Ngazija aliyeitwa Yusuf Hassan ambaye alikuwa Mwarabu, alizaa watoto wawili wa kiume, Hassan ‘Mbunsungulu’ na Ahmad. Wanasema kwamba Mufwimi alikuwa mmoja wa watoto watatu wa Mbunsungulu aliozaa na mwanamke wa Kikaguru. Ndugu zake wengine walikuwa Ngulusavangi na Ngwila, kwa maelezo yaliyo kwenye baadhi ya maandishi ambayo inatoweka kutokana na Watanzania kukosa utamaduni wa kutembea, kujifunza na kudadisi.
Rungemba ni kijiji ambacho hakijasikika sana katika historia kama lilivyo jina la Mkwawa, lakini hapa ndipo kwa kiasi kikubwa lilipo chimbuko la Chifu huyo wa kabila la Wahehe na ndipo lilipo kaburi la Mtwa Munyigumba.
Ignas Pangiligosi Muyinga, maarufu kama Malugila Mwamuyinga (61), ambaye ni kitukuu wa Msengele Kilekamagana, anaona fahari kuisimulia historia ya ukoo huo maarufu.
“Shina la ukoo wetu linaanzia kwa mtu aliyeitwa Mufwimi (yaani Mwindaji), ambaye mababu zetu walitusimulia kwamba alitokea Ethiopia,” Malugala anaanza kueleza. “Mufwimi alipita akiwinda kutoka Ethiopia, Kenya kabla ya kuingia Tanganyika na kujikuta yupo Usagara na hatimaye eneo la Nguluhe-Dabaga akipitia Ikombagulu, himaya ya Chifu Mwamududa. Wengi walimfananisha na mtu wa kabila la Wakamba kutoka Kenya kutokana na umbile lake kubwa.”
Wakati huo eneo ambalo sasa linaitwa Iringa lilikuwa na makabila mbalimbali. Walikuwepo ‘Wahafiwa’ katika Bonde la Milima Welu, Luvango, Wutinde, Lugulu, Makongati, Kalenga, Kipagala, Kihesa, Tambalang’ombe, Ibanagosi, Tipingi, Ikolofya, Nyambila, Kibebe na Isanzala.
‘Vanyategeta’ wao walioishi Udzungwa, Kitelewasi na Lundamatwe, ambao walikuwa wahunzi hodari. ‘Vanyakilwa’ walilowea Mufindi wakitokea Kilwa; ‘Vasavila’ waliishi milima ya Welu huko Makungu (Kihanga ya sasa),Magubike na Malangali; na ‘Vadongwe’ waliishi kando ya milima ya Uhambingeto, Ipogolo, Nyabula na Luhota.
Mufwimi alikuwa mwindaji mkubwa wa nyati ambapo aliichoma nyama yake kwa kuipaka chumvi ambayo ilikuwa haifahamiki kwa wakazi wa himaya hiyo, alimpelekea zawadi ya nyama-choma Chifu Mwamududa aliyeipenda mno kwa ladha yake.
Alipendwa na kukaribishwa na Mwamududa kuishi kwake, lakini akaanzisha mapenzi ya siri na Semduda, binti wa Chifu huyo, ambaye alikuwa amewakataa wachumba wengi. Binti huyo akapata ujauzito. Mufwimi akaogopa kwa kuona amefanya kosa kubwa. Jioni moja akamwita Semduda na kumweleza kwamba yeye anaondoka, lakini akampa maagizo, ikiwa atajifungua mtoto wa kike amwite Mng’anzagala na akiwa wa kiume amwite Muyinga Mufwimi (maana yake ni Mhangaikaji Mwindaji).
Mufwimi alitoroka kwa hofu ya kuuawa na Mwamududa. Akaendelea kuwinda huko na huko hadi Itamba alikouawa na nyati. Hakuna ajuaye lilipo kaburi lake.
Lakini kumbe mtawala huyo alifurahi kusikia bintiye ana mimba ya Mufwimi, maana alijua sasa angekubali kuolewa. Kwa bahati nzuri, binti huyo alijifungua mtoto wa kiume, hivyo akamwita jina la Muyinga Mufwimi kama alivyokuwa ameelekezwa na Mufwimi mwenyewe.
“Kijana huyo alipokua, kwa vile Chifu Mwamududa hakuwa na mtoto wa kiume, akaamua kuukabidhi utawala wake kwa mjukuu ambaye ni Muyinga Mufwimi aliyekuwa hodari wa vita. Kwa hiyo basi, uchifu huu wa Mkwawa ulitoka kikeni, na hapo ndipo uchifu ulipoanzia pamoja na ukoo wote maarufu wa Muyinga,” anafafanua Malugila.
Muyinga Mfwimi akaanza kutawala, akazaa watoto watatu wa kiume – Maliga, Nyenza na Mpondwa. Mtwa Maliga naye akazaa watoto watano wa kiume ambao ni Kitova, Mudegela, Mgayavanyi, Mkini na Kigwamumembe.
Inaelezwa kwamba, katika watoto wake hao, alisema Kitova yeye atakuwa tabibu (mganga wa tiba asilia) na Mudegela atakuwa mtawala, kwa maana hiyo Kitova alikuwa akitibu maradhi mbalimbali, lakini hasa majeruhi wa vita na kizazi chake ndicho kinachoendelea kutibu mifupa katika Kijiji cha Image mpaka sasa.
Mudegela Maliga yeye aliwazaa Lalika, Kalongole, Mbelevele, Wisiko, Kipaule, Mkanumkole, Lusoko na Mwakisonga. Hata hivyo, uchifu wake ulikwenda kwa mwanawe wa tano, ambaye ni Mtwa Kilonge.
Kilonge Mudegela alimuoa Maumba Sekindole aliyemzalia Ngawonalupembe na Munyigumba, lakini pia akamuoa Sekindole mwingine aliyewazaa Gunyigutalamu, mkewe wa tatu aliyeitwa pia Sekindole aliwazaa Magidanga, Mhalwike, Mupoma, Magoyo na Magohaganzali.

Hili ni kaburi la Mtwa Msengele Kilekamagana Munyigumba Mwamuyinga, mdogo wake Mtwa Mkwawa kwa Mama Sengimba mdogo. Picha zote na Admin.
“Kilonge alipofariki akazikwa katika eneo ambalo sasa ni Kijiji cha Lupembe lwa Senga (maana yake Pembe ya Ng’ombe), ambapo kaburi lake lilikuwa na pembe mbili za tembo, ingawa nasikia pembe zile ziliibwa na tunaambiwa walioiba wote walikufa ukoo mzima. Nasikia serikali ilipeleka pembe nyingine na kuzichimbia ili iwe kumbukumbu,” anasimulia Malugala.
Utawala una mambo yake, wakati mwingine unatumia njia halali na haramu ili kuudumisha. Malugala anasema, Munyigumba, ambaye ni mtoto wa pili wa Mtwa Kilonge, alihisi kwamba angeweza kuukosa uchifu kwa kumhofia kaka yake Ngawonalupembe.
“Kwa hiyo akafanya hila na kumuua kaka yake Ngawonalupembe ili yeye atawale, halafu akamchukua Sekinyaga, mke wa marehemu kaka yake kuwa mkewe, lakini wakati anamchukua, kumbe tayari Sekinyaga alikuwa mjamzito.
“Baada ya mtoto kuzaliwa, ambaye alikuwa wa kiume, Mama Sekinyaga akamwita Malangalila Gamoto, pengine kwa maelekezo ya marehemu Ngawonalupembe mumewe. Kwa hiyo Malangalila siyo mtoto wa Munyigumba, bali wa kaka yake ingawa yeye ndiye aliyemlea,” anaeleza Malugala.
Malugala anasimulia kwamba, ugomvi ulitokea baada ya mama huyo kujifungua ambapo alimwambia Munyigumba kwamba huyu siyo mtoto wake. Hapo Munyigumba akakasirika na kuamua kumfukuza Sekinyaga na mwanawe.
Inaelezwa kwamba, alipomfukuzwa, Sekinyaga akaelekea katika maeneo ya Sadani, lakini baadaye Munyigumba akajirudi kwa kuhisi angepata aibu, hivyo ikabidi amrudishe.
“Sasa wafuasi wake aliowatuma wakamchukue huyo mama wakaenda kumuua huko Sadani, hata kaburi lake halijulikani liliko. Wao wakarudi na mtoto Malangalila Gamoto. Kwa hiyo, Malangalila na Mkwawa ni mtu na mdogo wake kasoro baba zao,” anaeleza.
Munyigumba alikuwa na wake watano – Sengimba, Sendale, Sekinyaga (aliyekuwa mke wa kaka yake), Sembame na Sengimba mdogo. Sengimba mkubwa aliwazaa Kilemaganga, Mkwawa, Mpangile, Mulimbila na Wiyolitwe; Sendale alimzaa Mgungihaka; Sengimba mdogo alimzaa Msengele Kilekamagala; Sekinyaga alimzaa Malangalila Gamoto (kwa Ngawonalupembe); na Sembame alimzaa Mpugumoto.

USHUHUDA WA MWAKASEGE UNAGUSA SANA

Mwalimu Christopher Mwakasege
 Mwalimu Christopher Mwakasege alitoa ushuhuda huo katika semina iliyokuwa ikifanyika katika viwanja vya Furahisha jijini Mwanza Semina hiyo iliyokuwa  somo linaloitwa namna ambavyo Roho Mtakatifu awezavyo kukusaidia ili upokee kile unachokiomba.

Alisema Roho mtakatifu akwambiavyo omba hiyo haina MJADALA ni kuingia kwenye maombi mpaka upate unachokiomba kwa kuwa gharama ya kuingia kwenye maombi ili kupata ulichotakiwa kukipata ni ndogo kuliko gharama ya kukosa kile ulichoambiwa ukipate katika Maombi hayo.

Roho mtakatifu anapokupa mzigo wa kuombea jambo anakupa na muda ukizembea muda huo ukipita kinakuwa ni kiporo, na kiporo kinaweza kikalika na kipo ambacho hakiliki.  “Tulipoenda Israel na Fanuel Sedekia kisha akaanza kuumwa madaktari waliniambia ubongo wake kwa asilimia tisini haufanyi kazi. Lakini walishangaa kwa nini kila mara niko pale Hospitali wakasema kwa nini usikae tu Hotelini kisha ukawa unapiga simu kuulizia hali ya Mgonjwa? Wao hawakujua kwa nini naenda pale kwa kuwa suala la kupiga simu tu sio tatizo ningeweza kurudi Arusha kisha nikawa napiga simu.

Suala hapa ni kuwa nilikuwa naenda kila mara kwa ajili ya kumfanyia maombi, nilikuwa nakaa kandokando ya Bahari ya Galilaya nafanya maombi juu ya Sedikia kwa masaa sita nikitoka hapo nasikia upako wa ajabu sana kIsha napanda Taxi kuelekea
Hospitali. Nikifika Hospitali madactari na watu wa ICU walikuwa washanifahamu hivyo naenda moja kwa moja kwenye chumba cha nguo nabadili nguo kIsha naingia ICU alikolazwa.

Nikifika nambana Mungu kwa maswali Mengi namuuliza Sedekia, hivi unaongea nini na Yesu muda wote huo si urudi? na kisha namuuliza Yesu, hivi Yesu si unafahamu kuwa Sedekia anamke
ukimchukua mkewe atamuachia nani? Kisha baada ya maneno hayo naweka mkono juu yake.

Nilipokuwa nikiweka mkono juu yake ghafla upako wote unakuwa kama umenyonywa. Baada ya hapo narudi hotelini naanza tena
kumuuliza Mungu hivi Mungu kama basi husikii maombi yangu sikia maombi ya watanzania kwa kuwa saa hiyo nilijua watanzania wengi wanamuombea Sedekia.
Inafikia wakati nakata tamaa lakini ndani yangu najisemea Mwakasege haiwezekani jitie moyo kisha nabadili aina ya maombi, kwa kuwa nilikuwa na nguo zake pamoja na passport yake nikawa naviweka kati kisha nikawa naanza maombi ya Yeriko, nikawa niko hotelini usiku nazunguka nguo zake na paspot yake huku nikifanya maombi.

Taratibu Mungu akaanza kuniambia kuwa sedekia harudi, Kipidi hicho mimi na familia yangu tulikuwa tumepanga kwenda kupumzika nchini Uingereza wakati wa skukuu ya Chrismass, na booking mpaka ya Hotel tulikuwa tumeshafanya, na watoto wote wako nyumbani wakijiuliza tunaendaje kupumzika wakati Sedekia anaumwa? Chrismass ikapita na mwaka mpya pia kisha Sedekia akafariki.
Baada ya kifo hicho sikuchoka nkarudi tena kwa Mungu nikamuuliza kwa nini Mungu umeamua kumchukua Sedekia mikononi mwangu? Mungu alinijibu vitu ambavyo siwezi kuvisema hapa.

Kila siku mimi ni mgeni katika maombi namhitaji ROHO anifundishe kwa upya kwa kuwa sijui vita gani ninakwenda kupambana nayo, Mungu anabaki kuwa Mungu kwa kuwa hufanya atakavyo”
Ushuhuda huu umeandikwa kwenye facebook na Francisco. Unaweza kumfuatilia kwenye facebook hapa
---------------------------------------------------------------------------------
Kama una ushuhuda na ungetamani tuwashirikishe na wengine kupitia blogu yako ya Kikristo isiyofungamana na dhehebu lolote usiache kuwasiliana nasi kwenye facebook au tutumie kupitia ushuhudainjili@gmail.com

Mungu akubariki sana kwa kufuatana nasi.
Usiache kutufuatilia kwenye Facebook pamoja na Twitter