Mhalifu anapopigiwa saluti haki yaweza kupatikana kweli?
Ninaamini - na ushahidi uko upande wangu - Kamanda Kamuhanda alipaswa
kusimamishwa kazi mara moja, kushtakiwa katika mahakama ya kijeshi na
kuvuliwa vyeo vyake ili aweze kuunganishwa na watuhumiwa wengine (wale
waliompiga Mwangosi wanatakiwa pia wawemo).
KAMANDA wa Polisi wa Mkoa wa Iringa Michael Kamuhanda anastahili kutiwa
pingu na kufikishwa mahakamani akiunganishwa na mtuhumiwa nambari moja
wa mauaji ya Daud Mwangosi yaliyotokea siku kadhaa zilizopita.
Kushindwa kuchukuwa hatua mara moja dhidi ya Kamuhanda na uongozi wa
jeshi hilo na uongozi wa kisiasa nchini ni dalili mbaya zaidi ya
kuvunjika kwa mfumo wa utawala wa sheria.
Hili linanikumbusha kisa cha Ukiwaona Ditopile wa Mzuzuri (sasa
marehemu) na jinsi uongozi wa kisiasa ulivyojikuta unaweweseka katika
kuamua mizani ya haki iende vipi. Hata hivyo, ninaamini kuna sababu
kubwa mbili za kwanini kumchukulia hatua Kamanda Kamuhanda kumechelewa,
pengine kumetoa nafasi ya kuchezea ushahidi (tampering with evidence),
kutishia mashahidi (intimidation of witnesses) na kwa namna
yoyote kupindisha mwenendo wa uchunguzi na hivyo kuharibu mchakato wa
kupata haki (obstruction of justice).
Kwenye nchi ambayo inaheshimu utawala wa sheria kwa vile Kamanda
Kamuhanda alikuwa ni shuhuda wa tukio (material witness) hakupaswa kuwa
sehemu ya uchunguzi na kwa hakika hakupaswa kuendelea na wadhifa wake
wakati uchunguzi wa mauaji yaliyotokea mbele yake na kwa sababu yake
unafanyika.
Kumwacha aendelee na nafasi yake ni mojawapo ya uvunjaji mkubwa wa haki
ambao serikali imeruhusu na wanasiasa wetu wanavumilia. Sababu za
kwanini Kamuhanda asimamishwe kazi na kufunguliwa mashtaka (asili ya
mashtaka sitaki kuhisi sana lakini itakuwa ni kati ya matumizi mbaya ya
madaraka hadi mauaji) ni hizi zifuatazo. a. Hakuwa na sababu ya kuvunja
shughuli ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambayo ilikuwa
inafanyika kwa mujibu wa sheria.
Kwa wale walioona video ya mazungumzo yaliyotangulia vurumai kati ya
Kamuhanda na wandishi wa habari, hoja kubwa ilikuwa kama mkutano wa
CHADEMA ulikuwa ni "mkutano wa ndani" (internal meeting) au ulikuwa ni
mkutano uliokatazwa.
Wandishi wa habari - hasa marehemu Mwangosi - walisikika wakimpa nafasi
nyingi Kamuhanda kubadilisha njia. Kwamba maana ya
"internal meeting" si sawasawa na "inside meeting". Kwa maana ya kawaida
ya lugha ya Kingereza mkutano unaweza kuwani "internal" bila kuwa
"inside". Kwa kauli yake mwenyewe Kamanda Kamuhanda alifanya makosa
zaidi pale alipodai kuwa yeye ana haki ya kutafsiri sheria zote na si
kipengele kimoja.
Kwa kweli yeye si mtafsiri wa sheria na kama angekuwa na hekima (na
ushahidi unaonyesha kuwa hana)
alipaswa kuuliza mwanasheria wa serikali au mwanasheria mwingine kama
mkutano ule ambao ulikuwa ni "internal meeting" unalindwa na haukuwa
sehemu ya mikutano iliyopigwa marufuku. Kwa kutoa agizo la kuuvunja
mkutano ule Kamanda Kamuhanda - japo inaweza kuwa ni katika bona fide -
alivunja na kuingilia kati shughuli halali ya chama cha siasa kikifanya
mambo yake ya ndani.
Hakuwa na mamlaka, wala sababu ya kuingilia mkutano wa ndani na alikuwa
na nafasi ya kutosha kuweza kujihakikishia kuwa agizo lake lilikuwa
halali.
Kinyume cha watu wengine ambao wanataka kuwa CHADEMA walipaswa kutii
amri ya Polisi, binafsi naamini hawakutakiwa kutii amri hiyo ya kuwataka
waondoke kwa sababu haikuwa amri halali, haikuwahusu na kwa hakika
ilitolewa na mtu ambaye alitumia madaraka yake vibaya.
b. Wakati tukio la kuanza kumpiga mwandishi Mwangosi limeanza Kamanda
Kamuhanda alikuwa na haki na uwezo wa kuhakikisha haki za raia
zinalindwa.
Polisi wote wanajifunza sheria hii ambayo nimeweka hapo juu ambayo
inaelekeza wazi kuwa polisi wanapomkamata mtu au kumzuia mtu asiwatoroke
hawapaswi kutumia nguvu zaidi ya inayohitajika.
Yeye kama Kamanda wa Polisi wa Mkoa aliona nguvu ya Jeshi la Polisi
iliyokuwapo pale na kwa hakika hakukuwa na mtu hata mmoja ambaye alikuwa
ni tishio kwa jeshi hilo. Lakini zaidi ni kuwa walipomkamata Daud
Mwangosi hakuwa na kitu kingine chochote cha kutishia polisi zaidi ya
kamera na laptop yake. Wingi wa polisi waliomzunguka - picha na video
zinashuhudia - unathibitisha pasipo shaka kuwa kama polisi waliamini
(kwa sababu yoyote ile) kuwa Mwangosi amefanya kosa na
anastahili kuwekwa chini ya ulinzi, polisi walikuwa na uwezo na nguvu ya
kuweza kumdhibiti bila kumpiga.
Lakini kwa polisi kumkamata, kumpiga na hatimaye kumuua mbele ya Kamanda
wa Polisi wa Mkoa inathibitisha tu kuwa kamanda huyu hafai kuongoza
hata chipukizi!
Alitakiwa avuliwe vyeo vyake na kuwekwa kizuizini mara baada ya mauaji
yale ya Songea ambayo nayo yalitokea katika mazingira ya kutatanisha.
Lakini badala yake magenius wetu wa Taifa wakaona akajaribu kuongoza
Jeshi la Polisi kule Iringa.
Pamoja na hayo utaona kuwa hoja yangu inategemea sana kuwa kilichokiukwa
ni kifungu hicho cha 21 cha Mwenendo wa Makosa ya Jinai.
Kifungu hicho hata hivyo kinahusiana na tu na pale ambapo polisi
wanajaribu kumkatama mtu au kuzuia mtu asiwatoroke. Ukiangalia tukio la
mauaji ya Mwangosi ni wazi kuwa kilichotokea ni zaidi ya jaribio la
kumuweka mtu kizuizini au chini ya ulinzi.
Mahali ambapo pamezungukwa na polisi wa kila namna na wakiwa na silaha
ni mhalifu mjinga kabisa ambaye atajaribu kukimbia au ambaye hatotii
amri ya kuambiwa yuko chini ya ulinzi.
Picha za tukio lile zinaonyesha pasi ya shaka kuwa Mwangosi hakuwa kwa
namna yoyote ile ni mhalifu anayetaka kukimbia au ambaye ameamuriwa kuwa
chini ya ulinzi na akabisha.
Maelezo ya mashuhuda wote waliokuwapo kwenye tukio yanadai kuwa
kilichotokea kabla ya mauaji ni Mwangosi kupigwa kwanza na kundi la
polisi na kwa dakika kadhaa kabla ya kufyatuliwa bomu.
Kama hili ni kweli – na sidhani kama lina utata sana – mauaji ya
Mwangosi yanavuka maelekezo ya Kifungu hicho cha Sheria ya Mwenendo wa
Makosa ya Jinai kwa sababu kundi la polisi wakitumia madaraka wasiyo
nayo walianza kumpiga raia ambaye hakudaiwa uhalifu wowote na walifanya
hivyo mbele ya kiongozi mkuu wa polisi mkoani humo ambaye hakuna mtu
hata mmoja aliyejitokeza na kusema kuwa alijaribu kuzuia asipigwe!
Hii inanifanya niamini – na ninaomba msomaji ukubaliane
nami – kilichotokea pale ni kitendo cha uhalifu wa ugangwe wa kundi la
polisi ambao wakitumia silaha, sare na nafasi zao waliamini wanaweza
wakampiga raia yeyote bila kuulizwa.
Na uwepo wa kamanda Kamuhanda pale na ambaye alisababisha mtafaruku ule
kwa kutoa amri isiyo halali na kushindwa kwake kuingilia kati
kuhakikisha anaokoa maisha ya raia ni dalili kuwa kamanda huyo ni
mshirika wa uhalifu (criminal accomplice) na kumwacha aendelee kupigiwa
saluti, kushiriki vikao na kuendelea kuongoza Jeshi la Polisi mkoani
Iringa ni ucheleweshaji mkubwa wa haki, ni kukejeli akili za Watanzania
na kubeza kila namna ya kipimo cha utawala bora. Ni kumlinda mhalifu.
Je atafikishwa mahakamani? Kwa jinsi Polisi walivyochukulia hili na
zaidi wanasiasa wetu (wa chama tawala) walivyokubali hili ni wazi kuwa
Kamuhanda zaidi atakachofanywa ni kuhamishwa na kupelekwa mkoa mwingine
(ningependa binafsi aletwe
Dar es Salaam kuchukua nafasi ya Suleiman Kova).
Kumshtaki mtu mkubwa kama huyu ambaye ushahidi dhidi yake ni mkubwa
kuliko ule wa Abdallah Zombe na kesi ya wauza madini utatikisa Jeshi la
Polisi. Na kwa vile jeshi hili ni la kulindana (IGP Mwema ndiye
aliyemuhamisha kutoka Ruvuma!) ni wazi kuwa njia pekee ya kuja
kumshughulikia ni uongozi wa CHADEMA kuweka rekodi ya watendaji hawa ili
watakapoingia madarakani iwe ni watu wa kwanza
kushughulikiwa. Ikumbukwe mauaji hayana muda wa kukoma kuchunguzwa.
Ili kesi hii ionekane ina mfanano wa kudai haki kwa marehemu ni lazima
askari wote walioshiriki katika kumpiga marehemu (naweza kujenga hoja
kuwa yawezekana walimuua kabla ya bomu kulipuliwa!), baada ya askari
mlipuaji bomu kufikishwa mahakamani, sasa afuatie Kamanda Kamuhanda ili
kuonyesha kwamba Tanzania kuna mkono wa sheria usio na macho ya
upendeleo.
Lakini kwa vile tunajua hili ni gumu kufanyika – kama litafanyika
litazungushwa hadi kuondoa maana ya haki – basi Watanzania wajiwekee
dhamira kuwa hawa wote waliohusika siku moja watalipishwa.
Na watalipishwa pia wale wengine ambao wataendelea kutoa maisha ya wananchi kwa nguvu ili kujitafutia sifa kwa watawala.
No comments:
Post a Comment