Kwa mara nyengine tena Marekani imetangaza kuwa inapinga
Palestina kuwa mwanachama kamili katika Umoja wa Mataifa.Victoria Nuland,
msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani amesema Washington inapinga
juhudi mpya zinazofanywa na Wapalestina za kutaka Palestina itambulike kuwa
nchi huru katika Umoja wa Mataifa.
Siku chache nyuma, Mahmoud Abbas, Rais wa
Mamlaka ya Ndani ya Palestina aliwaambia waandishi wa habari huko mjini
Ramallah katika Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan kuwa tarehe 27 ya mwezi huu
wa Septemba atawasilisha tena ombi la uanachama wa Palestina katika Baraza Kuu
la Umoja wa Mataifa. Hivi sasa Palestina ni mwanachama mtazamaji tu katika
Umoja wa Mataifa asiye na uwezo wa kupiga kura, na matumaini ya viongozi wa
Kipalestina ni kuona wanachama wa umoja huo wanaikubali Palestina kuwa
mwanachama rasmi na kamili wa Umoja wa Mataifa.
Ombi la kutaka kutambuliwa
rasmi nchi huru ya Palestina mji mkuu wake ukiwa ni Baitul Muqaddas
liliwasilishwa na Mahmoud Abbas kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban
Ki-moon, lakini halikupasishwa kutokana na uungaji mkono wa kila hali wa
Marekani kwa utawala wa Kizayuni wa Israel, pingamizi za Washington ndani ya
Umoja wa Mataifa pamoja na msimamo dhaifu wa maafisa wa umoja huo. Hadi sasa
karibu nchi 140 zimetangaza kuwa zinaunga mkono mpango wa kuundwa nchi huru ya
Palestina. Katika miezi ya hivi karibuni Wapalestina wameanzisha kampeni kubwa
kwa lengo la kutaka Palestina itambuliwe kuwa nchi huru na Umoja wa Mataifa, na
juhudi hizo za Wapalestina kupigania haki yao hiyo zimepata uungaji mkono
mkubwa kimataifa.
Lakini hayo yanajiri katika hali ambayo katika kuendeleza upinzani
wake kwa juhudi hizo za kuhakikisha Wapalestina wanapata haki zao ikiwemo
kuunda nchi yao huru, Marekani inaweka vikwazo na pingamizi ili kufelisha na
kukwamisha tena juhudi za Wapalestina za kutaka kutangazwa kuundwa nchi huru ya
Palestina katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mnamo mwishoni mwa mwezi huu.
Marekani ndiyo nchi pekee inayopinga suala hilo, ambapo kwa kutumia kila aina
ya mbinu zikiwemo za kutishia kutumia kura yake ya veto dhidi ya ombi la
Wapalestina katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa imeviza na kufelisha
juhudi za Wapalestina za kutaka Baraza la Usalama lipasishe azimio la
kutambuliwa rasmi nchi huru ya Palestina. Vizuizi na pingamizi hizo za Marekani
zinakinzana kikamilifu na maazimio yaliyopasishwa na Umoja wa Mataifa ambayo
yanaunga mkono na kutilia mkazo haki za Wapalestina kujiamulia mustakabali wao
na kuwa na nchi yao huru.
Kuhusiana na nukta hiyo mwaka 2010 Baraza Kuu la
Umoja wa Mataifa lilipitisha kwa wingi mkubwa wa kura azimio la kuunga mkono
haki ya taifa la Palestina kujiamulia mustakabali wake. Azimio hilo
lilisisitiza na kutilia mkazo kwa mara nyengine tena haki ya wananchi wa
Palestina kuamua juu ya mustakabali wao ikiwemo kuwa na nchi yao huru.
Pamoja
na hayo hatua hiyo iliyochukuliwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na uungaji
mkono wa nchi nyingi duniani kwa haki za taifa la Palestina umekosolewa na
kulaumiwa na Marekani, ambayo ndiyo muungaji mkono mkuu wa utawala wa Kizayuni
wa Israel, kitendo ambacho kinadhihirisha upeo wa juu kabisa wa uadui wa
Washington kwa wananchi madhulumu wa Palestina
No comments:
Post a Comment