TATIZO HILI LA KAZAGAA KWA TAKA IRINGA VIONGOZI MNAONA? AU BADO MPO MPO KWANZA?
(Story kwa hisani ya Francisgodwin.blogspot.com)
Mwandishi wa makala haya Bw Fredrick Jailos anaanza
kwa kuhoji kuwa , Tumekosea Wapi?Tatizo la kuzagaa kwa taka taka
katika Manispaa ya Iringa mkoa wetu wa Iringa linakua kwa kasi kila
siku.
hili licha ya kua linaharibu sifa na hadhi ya mkoa wetu kama moja ya
mikoa misafi Tanzania, pia linahatarisha maisha ya viumbe hai -
binadamu, mimea, wanyama na viumbe vidogo kabisa (micro-organisms) Sifa
ya usafi kwa mkoa wa Iringa imedumu kwa miaka kadhaa, lakini kwa hali
ilivyo sasa, yawezekana sifa hiyo ikapotea.
Miaka kadhaa iliyopita, Iringa kulikua na makontena makubwa kwa ajili ya
kuhifadhia taka katika mitaa. Baada ya siku mbili tatu, gari lilipita
kubeba makontena hayo na kwenda kumwaga uchafu katika dampo la manispaa.
kontena lilirudishwa sehemu ile ile na wananchi wakaendelea kulitumia
kuhifadhi taka! Tatizo la kuzagaa kwa uchafu katika mitaa mbalimbali ya
mkoa wa Iringa kwa kiasi kikubwa lilipungua, na mji kuonekana msafi kwa
muda mwingi.
Zaidi ya makontena hayo, kuna baadhi ya mitaa ilijengewa vizimba kwa
ajili ya kuhifadhi takataka.Vizimba hivyo viliwezesha uchafu wa aina
tofauti kuhifadhiwa hapo mpaka siku ambayo gari itapita na kuukusanya.
Kwa hali ya sasa, vizimba hivyo vimekua vikiachwa kwa muda mrefu bila
kuondolewa takataka zilizorundikana ndani yake hivyo kusababisha
usumbufu kwa jamii zinazoishi karibu kabisa na vizimba kwani uchafu huo
hutoa harufu na kusambaa eneo lote la makazi
. Unapopita katika mitaa ya Iringa leo hii, utakuta hali tofauti!
Makontena mengi hayapo kwenye maeneo yaliyokuwepo na kusababisha
wananchi kutupa taka chini! Makontena ambayo yamebaki katika baadhi ya
maeneo hayatolewi mara kwa mara kwa ajili ya kwenda kumwagwa uchafu kama
ilivyokua zamani.
Hali hii inasababisha makontena hayo kujaa kupita kiasi, mpaka inafikia
hatua wananchi wanamwaga taka taka chini. Takataka hizo hukaa hapo kwa
muda mrefu mpaka kuja kutolewa.
Uwepo wa takataka hizo sehemu moja kwa muda mrefu husababisha harufu
mbaya katika eneo husika, na harufu hiyo husafiri mpaka kufikia umbali
wa mita 200 kutoka sehemu yenye uchafu.
Taka taka za plastiki, karatasi na chupa pia zinasafirishwa na upepo,
maji yanayotembea, na shughuli za binadamu kufikia mpaka umbali wa zaidi
ya mita 500 na kwenda kuchafua mazingira ya mitaa au maeneo mengine.
Ingawa kwa kiasi kidogo, lakini kuna taka za sumu (kemikali) zinazotupwa
katika vizimba na makontena yaliyoko sehemu za makazi (mf. Makopo ya
kemikali zinazotumika katika saluni za kiume na za kike).
Taka taka za namna hii zikikutana na jua na maji husababisha mmenyuko wa
kemikali (chemical reaction), na kupelekea uharibifu wa mazingira! Pia,
takataka za kemikali zinaweza kusafiri umbali mrefu ndani/chini ya
ardhi na kusababisha eneo kubwa kuathirika. Tatizo hili yawezekana
linasababishwa na mambo yafuatayo:
I. Ukosefu wa sheria ndogo ndogo zinazosimamiwa vizuri katika suala la uhifadhi wa taka.
II. Upungufu wa mapipa madogo ya kuhifadhia takataka katika mitaa mbalimbali ya mkoa wa Iringa.
III. Ongezeko la idadi ya watu wanaoishi ndani ya manispaa – hii
imesababisha kuongezeka kwa matumizi ya vitu/vifaa mbalimbali na
kuongeza wingi wa taka taka zinazozalishwa kwa siku.
IV. Kuchakaa kwa baadhi ya makontena ya kuhifadhia uchafu, pia kubomoka
kwa vizimba. Hii imesababisha upungufu wa vifaa hivyo, na kuwalazimu
wananchi katika baadhi ya mitaa kumwaga taka taka chini.
V. Ukosefu wa elimu ya mazingira kwa wananchi wa kawaida na kupelekea
matumizi mabaya ya vizimba na makontena ya kuhifadhia taka.
VI. Kutokua na utaratibu na usimamizi mzuri wa vizimba na makontena ya kuhifadhia uchafu.
\VII. Ratiba ya gari ya kuzoa taka haiko
wazi na haieleweki. Pia, kuna upungufu wa magari ya kufanya kazi hii.
VIII. Uzembe wa baadhi ya watendaji wa manispaa katika kusimamia suala la udhibiti wa taka.
NI NIN ATHARI ZA TAKATAKA HIZI. a. Uharibifu na Uchafuzi wa Mazingira.
b. Kusababisha magonjwa ya mlipuko. c. Kuharibu sifa na mandhari ya mji.
d. Kupunguza uwezo wa uzalishaji wa ardhi (rutuba) e. Kuchochea ukuaji
au mazalia ya vimelea vya magonjwa kwa wanyama na mimea mingine.
NINI KIFANYIKE? Kiujumla, suala la uhifadhi na usimamizi wa taka ni
suala linalohitaji pesa na maandalizi ya kutosha. Lakini kuna ulazima wa
suala hili kupewa uzito unaostahili ili Iringa, wananchi wake na viumbe
wengine waendelee kuwa salama. Baadhi ya mambo yanayoweza kusaidia
kupunguza tatizo hili ni pamoja na;
i. Kuwe na sheria ndogo zinazosimamiwa vizuri za uhifadhi wa taka
katika maeneo ya mjini. Sheria hizo zaweza kuwa sawa au zinazofanana na
zile zinazotumiwa katika mkoa wa Kilimanjaro katika uhifadhi wa taka
(Kwa Mkoa wa Kilimanjaro, ni marufuku kutupa taka taka hovyo, na hilo
linazingatiwa na wananchi kwani kuna usimamizi mzuri wa sharia hiyo
ndogo)
ii. Kuna haja ya kutafuta makontena zaidi na kuyaweka katika maeneo
mengi zaidi. Kutokana na kuongezeka kwa kasi kwa idadi ya watu mkoani
Iringa (kukichangiwa na uwepo wa vyuo vikuu vitatu), kuna haja ya
kuongeza idadi ya vizimba na makontena katika kila mtaa wa manispaa
yetu.
iii. Elimu ya uhifadhi wa taka itolewe kwa wananchi wa kawaida.
Serikali ya mkoa kwa kushirikiana na wadau wengine wa mazingira mkoani
Iringa (na kwingine) iandae mafunzo ya elimu ya uhifadhi wa taka kwa
ngazi ya kata na mitaa (wenyeviti, watendaji, mabalozi nk.). Elimu hii
inaweza kutolewa kwa viongozi wa kata na mitaa. Viongozi hao wawajibike
kuifikisha elimu hii kwa wananchi wa sehemu zao.
iv. Ushirikishwaji wa wadau wa mazingira katika program ndogo ndogo ni
muhimu. Kwa Mfano EBONY FM wamewahi kuwa na shughuli za kuchangisha pesa
kwa ajili ya kununua mapipa ya takataka kwa ajili ya mitaa ya Iringa
mjini. Wadau zaidi wakipewa mwamko, kutakuwa na unafuu kwa kiasi
kikukwa.
v. Ratiba ya gari ya kubeba taka iwekwe wazi kwa viongozi wa kata/mitaa
ili kupunguza tatizo la vizimba na makontena kujaa kupita kiasi.Kuwepo
na ratiba ya wazi kwa wananchi kuhusu siku za kukusanya takataka kwenye
mitaa. Kwa kila kizimba au mtaa, ziwepo siku maalumu za kukusanya taka,
na wananchi wa maeneo husika waambiwe siku hizo. Kwa kufanya hiyo
itasaidia katika kutoa taarifa pale gari ya kutoa takataka
itakaposhindwa kufika katika mtaa. Pia, inaweza kusaidia kwa wananchi
kujipangia utaratibu wa kupeleka taka katika vizimba na makontena.
vi. Kuna haja ya kuongeza gari za kuzolea taka ndani ya manispaa. Hii
inaweza kufanyika kwa manispaa kununua gari zaidi, au kutoa zabuni kwa
makampuni binafsi kwa ajili ya kazi hii.
vii. Kuna haja ya kuwa na mafunzo ya uhifadhi wa mazingira mashuleni.
Zaidi ya mitaala ya elimu inayozungumzia uhifadhi na usimamizi wa
mazingira, manispaa (kupitia idara au kitendo kinachojihusisha na
usimamizi na uhifadhi wa mazingira) wanaweza kuandaa program maalum ya
kupita mashuleni na kutoa elimu na mafunzo kuhusu uhifadhi wa taka. Kwa
njia hii, kaya nyingi za mitaa mingi zitafikiwa kiurahisi. Program hii
ihusishe shule za misingi na sekondari.
viii. Manispaa iwe na mtu/watu maalumu, ambaye ni mtaalamu wa mazingira
kwa ajili ya kuratibu na kusimamia shughuli za uhifadhi wa taka tu. Mtu
huyo anaweza kutoka katika kitengo cha mazingira au kuajiliwa. Kwa kuwa
na watu wa namna hiyo, itakuwa ni rahisi kufahamu hali ya mkoa wetu, na
pia kuwajibishana pale inapobidi.
ix. Utaratibu wa watu kupita nyumba kwa nyumba kukusanya uchafu mara
moja au mbili kwa wiki utasaidia kupunguza tatizo hili. Kila kaya
itatakiwa kuhifadhi taka taka zake, mpaka siku ambayo timu itapita
kuukusanya na kwenda kuutupa sehemu husika.
Kwa huduma hii, kila familia itatakiwa kulipia kiwango cha pesa
kitakachokubaliwa (mf. Tshs 500/ kwa kila familia). Hitimisho Miaka
kadhaa iliyopita Iringa ilikuwa inasifika kama mkoa msafi zaidi
Tanzania. Lakini kwa sasa hatupo tena kwenye nafasi hiyo.
Na hata kama tunaingia kwenye mikoa mitatu misafi zaidi nchini,
hatustahili kuwepo kwenye nafasi hiyo kwani hali yetu ni mbaya(Ingawa
walioko nyuma yetu wana hali mbaya zaidi). Tuna vichache vya kujivunia
katika suala la uhifadhi wa mazingira, alkini juhudi zaidi zinahitajika
ili kuurudisha mkoa kwenye heshima yake ya awali.
Tuangali tulipokosea na tujisahihishe kabla kipindupindu na magonjwa
mengine ya mlipuko hayajatushambulia. Ingawa jukumu hili linaonekana
kuwa la uongozi wa manispaa zaidi, lakini wananchi wanahusika kwa kiasi
kikubwa kulifanikisha hili.
Ushirikishwaji wa wananchi na wadau wengine (vyombo vya habari, AZAKI,
NK) katika uhifadhi wa taka, kuanzia ngazi ya kaya utasaidia kupunguza
tatizo hili kwa kiasi kikubwa. Hivyo basi, kuna haja ya manispaa
kujipanga upya katika mpango wake wa uhifadhi wa taka na kutia nguvu
zaidi sehemu zenye mapungufu. Tumepotea njia, ytunakoenda ni kule
tulipotoka miaka mingi iliyopita.
Hatua inayofuata ni kujipanga upya na kutafuta njia sahihi ya
kutufikisha tulipokuwa tunatakiwa kwenda. Mazingira safi na salama ni
haki ya kila mmoja wetu. Hivyo ni wajibu wa kila mwana Iringa
kuhakikisha kuwa anawajibika kuhifadhi mazingira hayo.
Na ili wajibu huu uwe sahihi, wananchi wafundishwe/waelekezwe ni nini
wanatakiwa kufanya ili tuendelee na safari kuelekea kwenye sifa ya mji
wenye mazingira safi na salama zaidi Tanzania.

mkazi wa Frelimo akitoka kutupa taka kata eneo hilo hilo ambalo taka zimezagaa

Kwa hali hii uongozi wa Manispaa ya Iringa akiwemo mbunge mchungaji
Peter Msigwa na wabunge wa viti maalum Ritta kabati (CCM) na Chiku
Abwao (chadema) sasa wanapaswa kuendelea kuimba wimbo wa usafi
katika mji wa Iringa .Haitoshi kwa viongozi hao wa kisiasa pia mkuu wa mkoa wa Iringa Dkt Ishengoma na katibu tawala Bi Mpaka pamoja na mkuu wa wilaya ya Iringa Dkt Warioba ambao kimsingi ni wakazi wa Manispaa ya Iringa hawana sababu ya kuendelea kuzichekea takataka hizo wanapaswa kushirikiana na mkurugenzi wa Manispaa ya Iringa na madiwani wa kata zote kuzichukia na kuzishughulikia vinginevyo mkoa wa Iringa utaongoza kwa aibu kwa ajili ya Manispaa ya Iringa .
No comments:
Post a Comment