Wameasi dini lakini maadili yako wapi
NIANZE makala hii kwa kurejea simulizi moja ambayo nimeshawahi kusimulia katika makala zilizopita.
Kati ya mambo yaliyonishangaza sana baada ya kuwasili hapa Uingereza kwa
mara ya kwanza, takriban muongo mmoja uliopita, ni jinsi Ukristo
ulivyopoteza
nguvu miongoni mwa Waingereza wengi.
Licha ya ‘kutolewa ushamba’ kwa kushuhudia vitu mbalimbali ambavyo kabla
ya kuja hapa vilikuwa ni vya kufikirika tu kama si kuviona kwenye
filamu na runinga, kilichoniacha mdomo wazi zaidi ni pale nilipoona
jengo ambalo zamani lilikuwa kanisa limegeuzwa klabu ya anasa za usiku
(night club).
Kwa Mndamba mie niliyezaliwa sehemu (Ifakara) ambayo ina historia ya
karibu na umisionari, kuona ‘nyumba ya Bwana’ imegeuzwa ukumbi wa anasa
lilikuwa jambo la kushangaza mno. Na kadri nilivyozidi kuielewa nchi hii
ndivyo
nilivyozidi kutambua kuwa idadi kubwa tu ya Waingereza haina muda na
Mungu au dini kwa ujumla.
Kila nilipopata wasaa wa kudadisi sikusita kuuliza swali hili, “hivi
imekuwaje ninyi mliotuletea Ukristo huko Afrika leo hii mnaonekana hamna
habari na dini hiyo ilhali dini inazidi kupamba moto huko kwetu?”
Majibu ya swali hilo yalikuwa tofauti kati ya mtu mmoja na mwingine,
lakini jibu lililojitokeza mara nyingi zaidi ni kuwa imani ya kiroho
haina nafasi muhimu katika zama hizi za sayansi na teknolojia.
Kimsingi, katika Jumapili ya kawaida, makanisa mengi ya Uingereza hujaza
‘wageni’ (kwa maana ya wakazi wenye asili ya nje ya nchi hii, hususan
Waafrika na Wakritso kutoka Ulaya ya Mashariki).
Katika siku za kati ya wiki, mengi ya makanisa hayo yamekuwa kama
vivutio vya utalii hasa ikizingatiwa kuwa mengi ya majengo hayo ya ibada
yana sehemu muhimu katika historia za sehemu yaliyopo.
Lakini ukidhani kufifia huko kwa ‘dini ya nchi hii’ (kimsingi Uingereza
ni nchi ya Kikristo na Malkia anaendelea kuwa ‘mkuu wa heshima’ wa
Kanisa la Anglikana duniani) kunawafanya Waingereza
kutokuwa watu wa kufuata maadili, basi ukienda sehemu mbalimbali za
huduma (kama vile kwenye benki, maduka makubwa nk) au ofisini utakumbana
na picha tofauti kabisa.
Kwanza, kwa kiasi kikubwa hakuna njia za mkato za kupata fedha katika
nchi hii pasipo kuwajibika. Pili, Waingereza wengi wanachukulia shughuli
zao kwa uzito na umuhimu mkubwa. Lakini jingine kubwa ni jinsi serikali
na taasisi za utawala zinavyojibidisha kutengeneza mazingira mazuri ya
kumwezesha kila anayejituma ‘avune matunda ya jasho lake.’
Kuna suala la haki na wajibu. Kwa kiwango kikubwa, wengi wa
Waingereza wanatambua wajibu wao wa kulipa kodi, na wajibu huo
unawapatia haki ya kupatiwa huduma ambazo kwa kiasi kikubwa zinakidhi
matakwa yao.
Kadhalika, taasisi mbalimbali za hapa zinatambua wajibu wao wa kutoa huduma zinazoendana na matakwa ya wahitaji huduma hizo.
Kwa hiyo, licha ya nafasi ya Mungu na Ukristo (au dini kwa ujumla)
kufifia miongoni mwa Waingereza wengi, bado kwa kiasi kikubwa jamii hii
inafanya ‘mema’ mengi zaidi ya akina sie huko nyumbani tusiokosekana
kwenye nyumba za ibada.
Binafsi, licha ya kutopendezwa kuona watu waliotuletea Ukristo huko
nyumbani ‘wakiupiga teke,’ wengi wa Waingereza wanaendelea kunivutia
jinsi wanavyoendesha maisha na shughuli zao kwa uadilifu mkubwa.
Japo Waingereza wengi ni kama hawana dini lakini wengi wao hawapo tayari
kuona mwanadamu mwingine ananyimwa haki zake za msingi, na ndiyo maana
nchi hii imetokea kuwa kimbilio kubwa kwa mamilioni ya wakimbizi ambao
miongoni mwao ni wale walionyanyaswa na kuteswa na nchi zao aidha kwa
imani au itikadi zao, jinsia zao, kutetea wanyonge na kadhalika.
Kwa hali hii, yayumkinika kuhitimisha kuwa bora kuwa ‘mpagani’ mtenda
mema kuliko mcha-Mungu fisadi. Ndiyo, dini imepoteza umuhimu wake kwa
wengi wa wenzetu hawa lakini wengi wao wameendelea kuwa ‘watu wema’
kuliko mamilioni ya wacha-Mungu huko Afrika.
Yawezekana kabisa ‘wapagani’ hawa kwenda mbinguni kutokana na kumpendeza
Mungu kwa matendo yao huku washika dini wetu wakigeuzwa kuni za
kuchochea washiriki wao katika kukandamiza, kuibia, kunyanyaswa na
kufanya kila baya kwa wanadamu wenzao.
Ni katika mazingira haya ya ‘Uingereza ninayoipenda licha ya wengi wa
watu wake kumpa kisogo
Mungu’ ndipo nilijikuta nikishtushwa na habari katika gazeti moja la
huko nyumbani kuwa Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Diane Louise
Corner, “amesifu serikali kwa kukuza demokrasia kutokana na uhuru
unaovipa vyombo vya habari kuujuza umma kuhusu mambo mbalimbali yakiwamo
matumizi ya umma yanayofanywa na serikali.”
Awali, naomba niseme bayana kuwa hadi muda huu bado nina wasiwasi iwapo
Balozi Corner alinukuliwa sahihi (yaani, iwapo kweli alitoa kauli hiyo).
Sitaki kabisa kuamini kuwa Balozi huyo hana taarifa kuhusu unyanyasaji mkubwa unaofanywa na serikali dhidi ya vyombo vya
habari binafsi huko nyumbani (ukiweka kando gazeti hilo la serikali liloandika habari hiyo).
Hivi inawezekana Balozi Corner hajawahi kusikia manyanyaso yaliyowakumba
wamiliki wa jukwaa huru la mtandaoni la Jamii Forums ambalo kwa hakika
limekuwa chanzo kikubwa cha kufichua maovu katika jamii?
Inawezekana Balozi huyo hajawahi kusikia tukio la kumwagiwa tindikali
kwa mwandishi wa habari Said Kubenea ambaye serikali inayosifiwa na
Balozi huyo imejipa jukumu la kudumu kumdhibiti mhariri huyo na gazeti
lake ambalo kwa sasa
limefungiwa kwa muda usiojulikana?
Ni demokrasia ipi anayozungumzia mwanadiplomasia huyo ambayo kwa upande
mmoja inaruhusu mikutano ya chama tawala CCM katika kampeni za uchaguzi
huko Zanzibar lakini si tu inapiga marufuku hata mikutano ya ndani ya
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) lakini pia inapelekea Jeshi
la Polisi kunyanyasa wananchi wasio na hatia ambao ‘kosa’ lao pekee ni
kutumia haki yao ya kikatiba na kidemokrasia ya kukusanyika (freedom of
association)?
Hivi kweli Balozi Corner hana taarifa kuwa Jeshi la Polisi limeshafanya
unyanyasaji mkubwa
dhidi ya wafuasi wa CHADEMA na kupelekea vifo vya wananchi wasio na
hatia huko Arusha, Morogoro na kubwa zaidi ni kifo cha mwandishi wa
habari Daudi Mwangosi huko Iringa hivi karibuni?
Ninasema sitaki kuamini kuwa uhuru wa vyombo vya habari au demokrasia
ninayoshuhudia hapa Uingereza ina tafsiri tofauti na hiyo anayosifia
Balozi huyo huko nyumbani.
Niwe mkweli, moja ya sababu ninazoona kuwa zinachangia sana ukosefu wa
utawala bora katika nchi zinazoendelea (ikiwamo Tanzania) ni tabia ya
nchi zilizoendelea kama Uingereza kuendeleza tabia ya kufumbia
macho ukiukwaji wa haki za binadamu ambao hauna nafasi kabisa katika
‘jamii zao za kistaarabu.’
Hivi majuzi tu, serikali ya Uingereza kupitia Waziri Mkuu David Cameron
imeomba msamaha kuhusiana na maafa ya Hillsborough yaliyotokea mwaka
1989 ambapo mashabiki kadhaa wa soka waliopoteza maisha.
Je, Balozi Corner anafahamu kuwa hadi leo serikali anayoisifia kwa
kukuza demokrasia haijaomba msamaha kwa japo kifo cha mwandishi Mwangosi
zaidi ya kuunda tume ambayo tayari imeanza kuhujumiwa huku baadhi ya
wajumbe wake wakilalamikiwa
kuwa na utendaji kazi wenye mushkeli?
Kama Mtanzania ninayeishi katika nchi ambayo huko nyuma ilitutawala kwa
mabavu lakini ninaiheshimu na kuipenda kwa mengi inayofanya kwa utu wa
mwanadamu pasi kujali ni Mwingereza au ‘mgeni,’ nimeshitushwa sana na
kauli ya Balozi Corner ambayo kimsingi inaweza kutumika kama sababu
tosha kwa watawala wetu kuendelea kukandamiza uhuru wa vyombo vya habari
na haki za binadamu kwa ujumla kwa kigezo cha kupewa ‘seal of approval’
na mwakilishi wa taifa kubwa na linaloaminika kwa kuenzi haki hizo
muhimu za binadamu.
Kuna nyakati ninapata shida sana kuyaelewa haya mataifa makubwa kama
Uingereza katika uhusiano wao na nchi ‘zinazojikongoja.’ Wao ndio
wafadhili wetu wakubwa, na asilimia ya kutosha ya fedha za walipakodi
wao ndizo zinachangia uhai na ustawi wa nchi masikini (japo zina utajiri
unaofilisiwa kila kukicha) kama Tanzania.
Lakini cha kushangaza, hakuna hatua za makusudi zinazochukuliwa nao
angalau kuwabana mafisadi wanaokwiba fedha zao (ambazo kimsingi
zinatolewa kwa minajili ya kumsaidia kila Mtanzania).
Sana sana ni utitiri wa sifa zinazomwagwa kwa watawala wetu
(kama hizo za kukuza demokrasia na uhuru wa vyombo vya habari), sifa
ambazo zinawapa motisha mafisadi kuendelea kuitafuna nchi yetu.
Je, ‘upole’ huo wa wafadhili wetu unachangiwa na hisia kuwa fedha za
mafisadi huishia kuhifadhiwa katika mabenki yaliyopo huku? Au
inawezekana bado mentality ileile iliyoleta ukoloni (na hata Ukristo)
kwamba sisi tulikuwa hatujastaarabika vya kutosha na ilikuwa muhimu kwa
wakoloni kujipa jukumu hilo, hadi sasa tunapaswa kuwa na demokrasia na
uhuru wa vyombo vya habari pungufu na tunayoshuhudia hapa Uingereza?
Nimalizie kwa kumkumbusha Balozi Corner kauli ya Waziri Mkuu wa
zamani wa Uingereza Gordon Brown katika harakati zake za kuisaidia Afrika.
Alisema (namnukuu katika tafsiri hii isiyo rasmi) “pasipo kuongeza
jitihada za kusaidia, itazigharimu baadhi ya nchi za Afrika zaidi ya
miaka 150 kufikia tulipofikia sisi (Waingereza).”
Lakini kwa mwenendo huu wa ‘sifa tusizostahili’ basi yayumkinika
kubashiri kuwa inaweza kutuchukua hata milele kufikia demokrasia ya
kweli yenye kuruhusu uhuru wa kweli wa vyombo vya habari.
No comments:
Post a Comment