ADVERT 1

ADVERT 1
Kilio na kimbilio la wanahabari Tanzania

Monday, October 15, 2012

TUMUENZI NYERERE KWA VITENDO


Wakati watanzania jana oktoba 14, wakijivunia kumuenzi Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wito watolewa juu ya namna bora ya kumuenzi .

Mmoja ya wanafamilia ya Mwalimu ndugu Vicent Nyerere yeye anasema " KILA mtu utamsikia akisema anamuenzi baba wa taifa Mw.Julius Kambarage Nyerere, kama tunamuenzi Mwalimu tumuenzi kwa vitendo kwa kufuata yale aliyokuwa akielekeza," 

Ni kweli tunavingi vya kujivunia na kumuenzi leo inapotimia miaka 13 tangu Nyerere aliyekuwa Rais wa kwanza wa taifa hili kufariki dunia October 14,1999 kwenye hospitali ya mtakatifu Thomas mji wa London nchini Uingereza alikokwenda kutibiwa kansa ya damu (leukemia).

Ama kwa hakika huu ni wakati wa huzuni kumkumbuka katika bara lote la Afrika na ulimwengu kwa ujumla, kutokana na jitihada zake za kutafuta uhuru, amani na mshikamano, taifa la Tanzania limepoteza kiongozi mwenye bidii na shupavu mwenye huruma 

Tukikumbuka kifo cha baba wa Taifa letu la Tanzania,tunamkumbuka  mwalimu kama mtu aliyejitahidi kutafuta amani katika ulimwengu mzima.

Nakumbuka ilikuwa ni siku  ya jumatatu ambapo Tanzania ilizizima baada ya mh Raisi wa awamu ya tatu Benjamin William Mkapa kuutangazia umma  akisema “ ndugu yetu,mpendwa wetu, baba yetu mwalimu wetu Julius kambarage Nyerere amefariki dunia”.

Vilio vilisikika kila mahala katika miji na vijiji vya Tanzania wakimlilia mkombozi wa nchi ya Tanzania kutoka katika makoloni ya kijerumani mnamo mwaka 1961

Siku tatu baadae watu walikusanyika Katika uwanja wa  ndege wa taifa jijini Dar-es-salam ili kushuhudia kile walichokisikia kwani ilikuwa ni ngumu kuamini kilichosika  mpaka mwili huo uliposhushwa toka nchini uingereza kwa ndege amambayo ilibeba mwili wa marehemu baba wa Taifa.

Tukimfananisha mwalimu na viongozi wengine wa leo ni nanani anayeweza kuikemea nchi kama Uingereza ama Marekani, akasikilizwa, achilia mbali mashirika ya kifedha ya kimataifa, kama Benki ya Dunia (WB) na IMF?. 

Nikinukuu toka katika gazeti la Raia mwema toleo no 156 la octoba 20,2010  mfano mmoja ni mwaka 1982, wakati Mwalimu aliposhikana shati na IMF akipinga shinikizo la shirika hilo kwa Tanzania kuridhia masharti na sera za kurekebisha uchumi (SAPs), ikiwa ni pamoja na kupunguza thamani ya fedha yake.  
Kiongozi walioonja hasira ya Mwalimu baada tu ya Uhuru mwaka 1961, alikuwa waziri wa sheria wa enzi hizo, Chifu Abdallah Fundikira aliyetuhumiwa kupokea rushwa. Hivyo, alifukuzwa uwaziri sawia.
 
Mwaka 1981, Mwalimu hakuweza kumwonea haya waziri wa mawasiliano, Augustine Mwingira, ilipobainika kuwa alinunua ndege mbovu kwa ajili ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATC), kutoka kwa mfanyabiashara wa Kipalestina, George Hallack; na kwamba ndege hiyo haikustahili bei iliyonunuliwa. Alimfukuza kazi, pamoja na meneja mkuu wa ATC, Lawrence Mmasi. Magofu ya ndege hiyo yanaonekana hadi leo uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius K. Nyerere.

Vivyo hivyo, mwaka huo, Mwalimu hakuweza kumvumilia Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Meli Tanzania (TSC) George Mbowe, ilipobainika kuwa alishiriki kumuuzia mfanyabiashara wa Kihindi, Akberali Rajpar, meli ya Shirika la Meli za Mwambao (TACOSHIL) – MV Jitegemee”, kwa bei ya kutupa na kwa mazingira ya kutatanisha.
Mbowe na meneja mkuu wa shirika hilo, Gideon Tibesigwa, walifukuzwa kazi; ambapo Rajpar alitiwa kizuizini kwa kipindi kwa tuhuma za kuhujumu uchumi.

Na aliyekuwa meneja mkuu wa Shirika la Vifaa vya Elimu (TES), Gervas Chilipweli, na mdhibiti wake wa fedha, Mujibur Rahman, walipumzishwa kazi baada ya kugunduliwa kwa hujuma na ubadhirifu mkubwa wa fedha katika shirika hilo.

Katika kipindi hicho hicho, Mwalimu alimfukuza kazi Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Abdulnuru Suleimani, kutokana na malalamiko ya wananchi juu ya kukithiri kwa rushwa katika uongozi wa mkoa.

Hebu tujiulize Leo, ni kiongozi gani mwenye ujasiri kama wa Mwalimu Nyerere, aliye tayari kusafisha nyumba yake kwa manufaa ya wanyonge na kuipatia heshima serikali yake?
Tangu awamu ya pili hadi ya nne ya uongozi wa nchi yetu, ni kiongozi gani ameweza kufumbia macho utajiri umpite kando na kujitoa mhanga kwa ajili ya anaowaongoza?. 

 Leo Tanzania, utajiri unanunua uongozi na uongozi unanunua utajiri; viongozi wa leo ni sehemu ya tabaka la matajiri wakubwa nchini, tofauti na enzi za uongozi wa Mwalimu Nyerere. Kitendo cha kuhalalisha “takrima” katika kampeni za kupata viongozi ni ushahidi tosha kwamba masikini hataweza tena kupata uongozi nchini kama hali hii itaendelea


Alikuwa kiongozi wa kanuni na mwenye msimamo usioyumba.
Kwa wakati huo watanzania walikuwa na imani kubwa na mwalimu kwa msimamo wake na vilevile sokoine kwa kuwa walikuwa ni wazalendo na nchi yao pia na huruma dhidi ya wananchi wanaowaongoza,ni kiongozi yupi leo, aliye tayari kwenda vijijini kuchanganyika na watu shambani, akawafundisha kilimo bora na jinsi ya kupambana na malaria?

Mwalimu aliweza kufanya hivyo; lakini “shangingi” za viongozi wa leo zinaogopa tope kuwafikia wanaovuja jasho mashambani. Kwa kifupi, Tanzania haijatoa kiongozi shupavu, mwadilifu na mahiri aina ya Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere.

Tunapoelekea kupata katiba mpya ya Tanzania, tuna kila sababu ya kujiuliza katika harakati za kujihakikishia uongozi bora: Nani kama Mwalimu Julius K. nyerere.
ambae mwishoni mwa maisha yake ataishi kama mkulima wa kawaida kama alivyo fanya kama mwalimu huko kijijini kwake Butiama. 

No comments:

Post a Comment