Katibu wa Baraza la Jumuiya za Kiislamu Ponda Issa Ponda alikamatwa
siku ya Jumanne kwa tuhuma za kuchochea ghasia na kuvunja amani jijini
Dar es Salaam, kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es
Salaam Suleiman Kova. Ponda aliitisha maandamano dhidi ya ardhi
iliyonunuliwa kutoka Baraza la Waislamu Tanzania na Kampuni ya
Agritanza.
Ponda pia anatuhumiwa kuchochea vurugu kufuatia mvulana mmoja kuikojolea Qu'ran
mapema wiki hii. Vile vile anatuhumiwa kuchochea maandamano haramu
miongoni mwa wafuasi wake juu ya kiwanja kilichouzwa kihalali, lakini
anasema lazima kibakie mikononi mwa Waislamu.
Idadi kubwa ya polisi wa Dar es Salaam walipelekwa katika wilaya ya
kibiashara katikati ya mji kuwadhibiti waandamanaji waliokerwa na
kukamatwa kwa Ponda. Waandamanaji wanne walikamatwa na polisi walitumia
gesi za machozi na magari ya maji kutawanya umati wa watu.
Mjini Zanzibar, vijana walitaka kujua taarifa za Sheikh Farid Hadi
Ahmed, kiongozi wa Jumuiya ya Maimamu visiwani humo, ambaye alitoweka
siku ya Jumanne.
Polisi hawajui alipo na wanachunguza kutoweka kwake, alisema kaimu
kamanda wa polisi wa mkoa wa Mjini/Magharibi Said Juma. Aliongeza kwamba
vijana wanaoandamana wameziba mitaa kwa mawe, taka na matairi
yaliyochomwa moto na wameunguza majengo.
No comments:
Post a Comment