Wakati watanzania jana oktoba 14, wakijivunia kumuenzi Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wito watolewa juu ya namna bora ya kumuenzi .
Mmoja ya wanafamilia ya Mwalimu ndugu Vicent Nyerere yeye anasema " KILA
mtu utamsikia akisema anamuenzi baba wa taifa Mw.Julius Kambarage
Nyerere, kama tunamuenzi Mwalimu tumuenzi kwa vitendo kwa kufuata yale
aliyokuwa akielekeza,"
Ni kweli tunavingi vya kujivunia na kumuenzi leo inapotimia miaka 13 tangu
Nyerere aliyekuwa Rais wa kwanza wa taifa hili
kufariki dunia October 14,1999 kwenye hospitali ya mtakatifu Thomas mji wa London nchini
Uingereza alikokwenda kutibiwa kansa ya damu (leukemia).
Ama kwa hakika huu ni wakati wa huzuni kumkumbuka katika
bara lote la Afrika na ulimwengu kwa ujumla, kutokana na jitihada zake za kutafuta uhuru, amani na mshikamano, taifa la Tanzania limepoteza kiongozi
mwenye bidii na shupavu mwenye huruma
Tukikumbuka
kifo cha baba wa Taifa letu la Tanzania,tunamkumbuka mwalimu kama mtu
aliyejitahidi kutafuta amani katika ulimwengu mzima.
Nakumbuka ilikuwa ni siku ya jumatatu ambapo Tanzania ilizizima baada ya mh
Raisi wa awamu ya tatu Benjamin William Mkapa kuutangazia umma akisema “ ndugu yetu,mpendwa wetu, baba yetu
mwalimu wetu Julius kambarage Nyerere amefariki dunia”.
Vilio vilisikika kila mahala katika miji na
vijiji vya Tanzania
wakimlilia mkombozi wa nchi ya Tanzania
kutoka katika makoloni ya kijerumani mnamo mwaka 1961
Siku tatu baadae watu walikusanyika Katika uwanja wa ndege wa taifa jijini Dar-es-salam ili
kushuhudia kile walichokisikia kwani ilikuwa ni ngumu kuamini kilichosika mpaka mwili huo uliposhushwa toka nchini
uingereza kwa ndege amambayo ilibeba mwili wa marehemu baba wa Taifa.
Tukimfananisha
mwalimu na viongozi wengine wa leo ni nanani anayeweza kuikemea nchi kama
Uingereza ama Marekani, akasikilizwa, achilia mbali mashirika ya kifedha ya
kimataifa, kama Benki ya Dunia (WB) na IMF?.
Nikinukuu toka katika gazeti la Raia mwema toleo no 156 la
octoba 20,2010 mfano mmoja ni mwaka
1982, wakati Mwalimu aliposhikana shati na IMF akipinga shinikizo la shirika hilo kwa Tanzania
kuridhia masharti na sera za kurekebisha uchumi (SAPs), ikiwa ni pamoja na
kupunguza thamani ya fedha yake.
Kiongozi walioonja hasira ya Mwalimu
baada tu ya Uhuru mwaka 1961, alikuwa waziri wa sheria wa enzi hizo, Chifu
Abdallah Fundikira aliyetuhumiwa kupokea rushwa. Hivyo, alifukuzwa uwaziri
sawia.
Mwaka 1981, Mwalimu hakuweza kumwonea
haya waziri wa mawasiliano, Augustine Mwingira, ilipobainika kuwa alinunua
ndege mbovu kwa ajili ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATC), kutoka kwa
mfanyabiashara wa Kipalestina, George Hallack; na kwamba ndege hiyo
haikustahili bei iliyonunuliwa. Alimfukuza kazi, pamoja na meneja mkuu wa ATC,
Lawrence Mmasi. Magofu ya ndege hiyo yanaonekana hadi leo uwanja wa ndege wa
kimataifa wa Mwalimu Julius K. Nyerere.
Vivyo hivyo, mwaka huo, Mwalimu hakuweza
kumvumilia Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Meli Tanzania (TSC)
George Mbowe, ilipobainika kuwa alishiriki kumuuzia mfanyabiashara wa Kihindi,
Akberali Rajpar, meli ya Shirika la Meli za Mwambao (TACOSHIL) – MV Jitegemee”,
kwa bei ya kutupa na kwa mazingira ya kutatanisha.
Mbowe na meneja mkuu wa shirika hilo, Gideon Tibesigwa,
walifukuzwa kazi; ambapo Rajpar alitiwa kizuizini kwa kipindi kwa tuhuma za
kuhujumu uchumi.
Na aliyekuwa meneja mkuu wa Shirika la
Vifaa vya Elimu (TES), Gervas Chilipweli, na mdhibiti wake wa fedha, Mujibur
Rahman, walipumzishwa kazi baada ya kugunduliwa kwa hujuma na ubadhirifu mkubwa
wa fedha katika shirika hilo.
Katika
kipindi hicho hicho, Mwalimu alimfukuza kazi Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Abdulnuru
Suleimani, kutokana na malalamiko ya wananchi juu ya kukithiri kwa rushwa
katika uongozi wa mkoa.
Hebu tujiulize Leo, ni kiongozi gani mwenye ujasiri kama wa Mwalimu Nyerere, aliye tayari kusafisha nyumba
yake kwa manufaa ya wanyonge na kuipatia heshima serikali yake?
Tangu
awamu ya pili hadi ya nne ya uongozi wa nchi yetu, ni kiongozi gani ameweza
kufumbia macho utajiri umpite kando na kujitoa mhanga kwa ajili ya
anaowaongoza?.
Leo Tanzania, utajiri unanunua uongozi na uongozi unanunua
utajiri; viongozi wa leo ni sehemu ya tabaka la matajiri wakubwa nchini,
tofauti na enzi za uongozi wa Mwalimu Nyerere. Kitendo cha kuhalalisha
“takrima” katika kampeni za kupata viongozi ni ushahidi tosha kwamba masikini
hataweza tena kupata uongozi nchini kama hali
hii itaendelea
Alikuwa kiongozi wa kanuni
na mwenye msimamo usioyumba.
Kwa wakati huo watanzania walikuwa na
imani kubwa na mwalimu kwa msimamo wake na vilevile sokoine kwa kuwa walikuwa
ni wazalendo na nchi yao
pia na huruma dhidi ya wananchi wanaowaongoza,ni kiongozi yupi leo, aliye
tayari kwenda vijijini kuchanganyika na watu shambani, akawafundisha kilimo
bora na jinsi ya kupambana na malaria?
Mwalimu
aliweza kufanya hivyo; lakini “shangingi” za viongozi wa leo zinaogopa tope
kuwafikia wanaovuja jasho mashambani. Kwa kifupi, Tanzania haijatoa kiongozi shupavu,
mwadilifu na mahiri aina ya Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere.
Tunapoelekea kupata katiba mpya ya Tanzania, tuna kila
sababu ya kujiuliza katika harakati za kujihakikishia uongozi bora: Nani kama
Mwalimu Julius K. nyerere.
ambae mwishoni
mwa maisha yake ataishi kama mkulima
wa kawaida kama alivyo fanya kama mwalimu huko kijijini kwake Butiama.