ADVERT 1

ADVERT 1
Kilio na kimbilio la wanahabari Tanzania

Wednesday, November 13, 2013


MWILI WA DKT. SENGONDO MVUNGI KUWASILI IJUMAA NOVEMBA 15 2013, KINANA AMLILIA 

 

 Rais Jakaya Kikwete akitia saini kitabu cha maombelezo ya kifo cha Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Dkt. Sengondo Mvungi nyumbani kwake Kibamba jijini Dar es Salaam.
  Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Joseph Warioba wakifurahia jambo na Waziri wa Katiba na Sheria Mathias Chikawe (kushoto), Makamu Mwenyekiti wa Tume Jaji Mkuu Mstaafu Augustino Ramadhani na Mjumbe wa Tume Waziri Mkuu Mstaafu Dkt. Salim Ahmed Salim (kulia) walipokutana nyumbani kwa marehemu Dkt. Sengondo Mvungi Kibamba jijini Dar es Salaam.
(Picha na Tume ya Katiba)
  Rais Jakaya Kikwete (katikati) akibadilishana mawazo na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Joseph Warioba (kushoto) nyumbani kwa marehemu Dkt. Sengondo Mvungi walipokwenda kuipa pole familia. Kulia ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi James Mbatia na Mjumbe wa Tume Waziri Mkuu Mstaafu Dkt. Salim Ahmed Salim.
 Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Richard Lyimo akimpa pole mke wa marehemu Dkt. Sengondo Mvungi, Bi. Anna Mvungi wakati Wajumbe wa Tume walipokwenda kumpa pole.
  Rais Jakaya Kikwete akimpa pole mke wa marehemu Dkt. Sengondo Mvungi, Bi. Anna Mvungi alipokwenda kumpa pole nyumbani kwake Kibamba jijini Dar es Salaam.
 wenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Joseph Warioba wakifurahia jambo na Waziri wa Katiba na Sheria Mathias Chikawe (kushoto), Makamu Mwenyekiti wa Tume Jaji Mkuu Mstaafu Augustino Ramadhani na Mjumbe wa Tume Waziri Mkuu Mstaafu Dkt. Salim Ahmed Salim (kulia) walipokutana nyumbani kwa marehemu Dkt. Sengondo Mvungi Kibamba jijini Dar es Salaam.
(Picha na Tume ya Katiba)
.............................................................................................................................
Tume ya Mabadiliko ya Katiba inawafahamisha wananchi kuwa taratibu za kuusafirisha mwili wa Mjumbe wake, Dkt. Sengondo Mvungi aliyefariki nchini Afrika Kusini zimekamilika na mwili wake unatarajia kuwasili nchini siku ya Ijumaa, Novemba 15, 2013.

Baada ya kuwasili, mwili huo utahifadhiwa katika Hospitali ya Jeshi Lugalo iliyopo jijini Dar es Salaam.

Aidha, siku ya Jumamosi, Novemba 16, 2013 kutafanyika Ibada ya mazishi katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph jijini Dar es Salaam kuanzia saa 4:00 asubuhi. Baada ya misa, marehemu ataagwa katika Viwanja vya Karimjee kuanzia saa 6:30 mchana siku hiyohiyo ya Jumamosi, Novemba 16, 2013.

Aidha, Marehemu Dkt. Mvungi anatarajiwa kusafirishwa siku ya Jumapili, Novemba 17, 2013 kwenda Kisangara Juu, Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya mazishi yanayotarajiwa kufanyika siku ya Jumatatu, Novemba 18, 2013.

Dkt. Mvungi alifariki jana (Jumanne, Novemba 12, 2013) katika Hospitali ya Millpark jijini Johannesburg nchini Afrika Kusini alikopelekwa kwa ajili ya uchunguzi na matibabu zaidi akitokea Kitengo cha Mifupa Muhimbili (MOI) aliokuwa amelazwa baada ya kuvamiwa nyumbani kwake Kibamba, wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam na watu waliomjeruhi vibaya kichwani usiku wa kuamkia siku ya Jumapili, Novemba 3, 2013.

Wakati huohuo, Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba wakiongozwa na Mwenyekiti wake Jaji Joseph Warioba leo (Jumatano, Novemba 13, 2013) wameungana na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kufika nyumbani kwa marehemu Dkt. Mvungi eneo la Kibamba jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kutoa pole kwa familia, ndugu na jamaa wa marehemu Dkt. Mvungi.
Mwisho.
Imetolewa na:
Ndg. Assaa A. Rashid,
Katibu,
Tume ya Mabadiliko ya Katiba,
Dar es Salaam

 
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ndugu Abdulrahaman Kinana amesikitishwa na taarifa ya kifo Cha Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Dr Sengondo Mvungi kilichotokea Jana katika Hospitali ya Millpark nchini Afrika ya Kusini.

Kwa niaba ya Chama Cha Mapinduzi, Katibu Mkuu anawapa pole wanafamilia, Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Warioba na Uongozi wa Chama Cha NCCR-Mageuzi. Hakika Taifa limepoteza Mtaalamu wa Sheria, Kiongozi Mzalendo na hodari katika kipindi ambacho mawazo yake yanahitajika kwa kiasi kikubwa kuliendeleza Taifa hili.
Mwenyezi Mungu aiweke roho ya marehemu mahali pema peponi.
Imetolewa na:
KATIBU WA HALMASHAURI KUU YA TAIFA
ITIKADI NA UENEZI
13/11/2013
 
Habari kwa hisani ya www.francisgodwin.blogspot.com
Mwalimu Nyerere na Sheikh Karume

 Mwl Nyerere wenzio wanavunja Muungano


Na DANIEL MBEGA
Salaam Mwalimu Nyerere,
Sina shaka kwamba huko uliko umepumzika kwa amani, kwa uwezo wa Mungu. Yawezekana umekuwa mwenyeji huko na kazi yako njema uliyoifanya katika kuhakikisha Tanganyika inajitawala, na hatimaye inaungana na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar kuzaa Tanzania, bado ni kitambulisho tosha ndiyo maana leo hii, miaka 14 baada ya kifo chako, bado Watanzania tunakukumbuka huku duniani.
Lakini nina uhakika hujui yanayotokea huku Tanzania. Kwa kifupi, mambo yameharibika. Natamani waraka wangu ungekufikia mwenyewe mkononi ili nikukumbushe ama nikupashe yanayoendelea huku.
Wale wote uliowanadi mwaka 1995 ili waienzi Ikulu yetu, walikugeuka miezi michache tu baada ya wewe kulala na babu zako. Wakaigeuza Ikulu kuwa sehemu ya biashara – ingawa wapo wengine uliwauliza “…Mnakimbilia Ikulu kufanya biashara gani!” Viwanda vyote ulivyopigania kuanzishwa waauziana wenyewe. Ikulu ikawa sehemu ya kusaini mikataba mibovu ambayo immeshuhudia madini yetu yalikuvunwa na kupelekwa nje huku sisi tukibaki na mashimo tu.
Kwa kifupi, uliona wanafaa walikusailiti. Maadili ya uongozi uliyoyasisitiza yakatoweka. Vita ya rushwa imeshindikana kwani wenye dhamana ya kupambana nayo ndio vinara wa kutoa na kupokea rushwa. Natamani hata Chifu Fundikira angekuwepo naye aone wenzake wanavyofaidi – pengine angesikitika kwa nini yeye aliondolewa kwenye Baraza lako la Mawaziri miaka michache tu baada ya uhuru.
Ufisadi umetamalaki kila kona, chaguzi zimegubikwa na rushwa mbaya. Chama chako cha Mapinduzi kimekuwa ‘Chama cha Matajiri’. Bora hili ni neon zuri, lakini wengine wanakiita ‘Chama cha Mafisadi’, au ‘Chama cha Majangili’ na wengine wanathubutu kusema ni ‘Chama cha Majambazi’, ilimradi kila mmoja anatamka neno analoona linafaa. Maskini hawana nafasi, wachache tu ndio wana sauti kwa sababu ya fedha zao.
Wale uliowapinga ndani ya Chama wakati ule, uliowahoji kuhusu walikopata utajiri wao, leo hii ndio wanaoabudiwa. Mbaya zaidi wanapita mpaka misikitini na makanisani kutoa misaada, halafu wanapigiwa makofi na kuimbiwa mapambio. Ungewaona, nina imani ungemwaga machozi. Naamini mama yetu Maria anaugulia moyoni kwa yanayotokea.
Mwalimu, sikuwepo wakati huo, lakini nakumbuka ilikuwa Jumapili, Aprili 26, 1964, saa 4.00 asubuhi wakati wewe – ukiwa Mwenyekiti wa TANU – ulipokutana na Mwenyekiti wa Afro-Shiraz Party (ASP) Sheikh Abeid Amani Karume mjini Dar es Salaam na kusaini hati ya makubaliano ya kuziunganisha nchi zenu. Muungano huu ulifikiriwa kwa takribani miezi mitatu na siku 24 tu tangu yalipofanyika mapinduzi ya kuung’oa utawala dhalimu wa Kisultani visiwani Zanzibar Januari 12, 1964. Kabla ya kutiwa saini, nyote wawili mlikuwa mmefanya mazungumzo mara kadhaa mjini Dar es Salaam na Unguja na ndipo mkafikia mwafaka wa kuziunganisha nchi hizo.
Wapo walioupinga wakati huo (na wanaendelea kuupinga) kwamba haukufuata misingi inayotakiwa katika muungano halisi, lakini pia wapo walioufurahia na wanaendelea kuufurahia kwa kuwa umeleta udugu na kujenga umoja na mshikamano.
Mwalimu, imebaki miezi michache tu ili Muungano huu utimize miaka 50, lakini nina mashaka kama hautakufa kabla ya miaka hiyo kutimia. Umoja, amani, upendo na mshikamano uliojengwa na muungano huo umetoweka kabisa.

Mpiganaji wa ukweli na kiongozi wa kabila dogo la wahehe aliyetikisa Ujerumani




Hili ni kaburi la Mtwa Munyigumba Kilonge Mdegella Mwamuyinga lililo katika Kijiji cha Rungemba wilayani Mufindi, takribani kilometa 61 kutoka Iringa mjini.

Na Daniel Mbega
MAANDIKO kadhaa yamekuwepo kuhusiana na historia ya Wahehe na hasa ukoo wa Mtwa Mkwavinyika Munyigumba Mwamuyinga, maarufu kama Mkwawa, lakini yote hayo hayakunizuia kuisaka historia hiyo.
‘Jicho halishibi kuona na Sikio halikinai kusikia!’ hivyo nikaamua kufunga safari hadi Lungemba, yaliko makaburi ya Mtwa Munyigumba na ndugu wengine wa ukoo huo, yapata kilometa 62 kutoka Iringa Mjini.
Wapo walioandika kwamba chimbuko la Mtwa Mkwawa ni Ungazija, lakini simulizi ninazokutana nazo hapa ni tofauti, maana zinatoka katika vinywa vya wanaukoo wa Muyinga, ambao nao wameipata ama kurithishwa kutoka kizazi na kizazi kutokana na simulizi za mababu zao.
Wale waliopata kuandika kwamba asili ya akina Mkwawa ni Ungazija wanaeleza kuwa mtawala wa Ngazija aliyeitwa Yusuf Hassan ambaye alikuwa Mwarabu, alizaa watoto wawili wa kiume, Hassan ‘Mbunsungulu’ na Ahmad. Wanasema kwamba Mufwimi alikuwa mmoja wa watoto watatu wa Mbunsungulu aliozaa na mwanamke wa Kikaguru. Ndugu zake wengine walikuwa Ngulusavangi na Ngwila, kwa maelezo yaliyo kwenye baadhi ya maandishi ambayo inatoweka kutokana na Watanzania kukosa utamaduni wa kutembea, kujifunza na kudadisi.
Rungemba ni kijiji ambacho hakijasikika sana katika historia kama lilivyo jina la Mkwawa, lakini hapa ndipo kwa kiasi kikubwa lilipo chimbuko la Chifu huyo wa kabila la Wahehe na ndipo lilipo kaburi la Mtwa Munyigumba.
Ignas Pangiligosi Muyinga, maarufu kama Malugila Mwamuyinga (61), ambaye ni kitukuu wa Msengele Kilekamagana, anaona fahari kuisimulia historia ya ukoo huo maarufu.
“Shina la ukoo wetu linaanzia kwa mtu aliyeitwa Mufwimi (yaani Mwindaji), ambaye mababu zetu walitusimulia kwamba alitokea Ethiopia,” Malugala anaanza kueleza. “Mufwimi alipita akiwinda kutoka Ethiopia, Kenya kabla ya kuingia Tanganyika na kujikuta yupo Usagara na hatimaye eneo la Nguluhe-Dabaga akipitia Ikombagulu, himaya ya Chifu Mwamududa. Wengi walimfananisha na mtu wa kabila la Wakamba kutoka Kenya kutokana na umbile lake kubwa.”
Wakati huo eneo ambalo sasa linaitwa Iringa lilikuwa na makabila mbalimbali. Walikuwepo ‘Wahafiwa’ katika Bonde la Milima Welu, Luvango, Wutinde, Lugulu, Makongati, Kalenga, Kipagala, Kihesa, Tambalang’ombe, Ibanagosi, Tipingi, Ikolofya, Nyambila, Kibebe na Isanzala.
‘Vanyategeta’ wao walioishi Udzungwa, Kitelewasi na Lundamatwe, ambao walikuwa wahunzi hodari. ‘Vanyakilwa’ walilowea Mufindi wakitokea Kilwa; ‘Vasavila’ waliishi milima ya Welu huko Makungu (Kihanga ya sasa),Magubike na Malangali; na ‘Vadongwe’ waliishi kando ya milima ya Uhambingeto, Ipogolo, Nyabula na Luhota.
Mufwimi alikuwa mwindaji mkubwa wa nyati ambapo aliichoma nyama yake kwa kuipaka chumvi ambayo ilikuwa haifahamiki kwa wakazi wa himaya hiyo, alimpelekea zawadi ya nyama-choma Chifu Mwamududa aliyeipenda mno kwa ladha yake.
Alipendwa na kukaribishwa na Mwamududa kuishi kwake, lakini akaanzisha mapenzi ya siri na Semduda, binti wa Chifu huyo, ambaye alikuwa amewakataa wachumba wengi. Binti huyo akapata ujauzito. Mufwimi akaogopa kwa kuona amefanya kosa kubwa. Jioni moja akamwita Semduda na kumweleza kwamba yeye anaondoka, lakini akampa maagizo, ikiwa atajifungua mtoto wa kike amwite Mng’anzagala na akiwa wa kiume amwite Muyinga Mufwimi (maana yake ni Mhangaikaji Mwindaji).
Mufwimi alitoroka kwa hofu ya kuuawa na Mwamududa. Akaendelea kuwinda huko na huko hadi Itamba alikouawa na nyati. Hakuna ajuaye lilipo kaburi lake.
Lakini kumbe mtawala huyo alifurahi kusikia bintiye ana mimba ya Mufwimi, maana alijua sasa angekubali kuolewa. Kwa bahati nzuri, binti huyo alijifungua mtoto wa kiume, hivyo akamwita jina la Muyinga Mufwimi kama alivyokuwa ameelekezwa na Mufwimi mwenyewe.
“Kijana huyo alipokua, kwa vile Chifu Mwamududa hakuwa na mtoto wa kiume, akaamua kuukabidhi utawala wake kwa mjukuu ambaye ni Muyinga Mufwimi aliyekuwa hodari wa vita. Kwa hiyo basi, uchifu huu wa Mkwawa ulitoka kikeni, na hapo ndipo uchifu ulipoanzia pamoja na ukoo wote maarufu wa Muyinga,” anafafanua Malugila.
Muyinga Mfwimi akaanza kutawala, akazaa watoto watatu wa kiume – Maliga, Nyenza na Mpondwa. Mtwa Maliga naye akazaa watoto watano wa kiume ambao ni Kitova, Mudegela, Mgayavanyi, Mkini na Kigwamumembe.
Inaelezwa kwamba, katika watoto wake hao, alisema Kitova yeye atakuwa tabibu (mganga wa tiba asilia) na Mudegela atakuwa mtawala, kwa maana hiyo Kitova alikuwa akitibu maradhi mbalimbali, lakini hasa majeruhi wa vita na kizazi chake ndicho kinachoendelea kutibu mifupa katika Kijiji cha Image mpaka sasa.
Mudegela Maliga yeye aliwazaa Lalika, Kalongole, Mbelevele, Wisiko, Kipaule, Mkanumkole, Lusoko na Mwakisonga. Hata hivyo, uchifu wake ulikwenda kwa mwanawe wa tano, ambaye ni Mtwa Kilonge.
Kilonge Mudegela alimuoa Maumba Sekindole aliyemzalia Ngawonalupembe na Munyigumba, lakini pia akamuoa Sekindole mwingine aliyewazaa Gunyigutalamu, mkewe wa tatu aliyeitwa pia Sekindole aliwazaa Magidanga, Mhalwike, Mupoma, Magoyo na Magohaganzali.

Hili ni kaburi la Mtwa Msengele Kilekamagana Munyigumba Mwamuyinga, mdogo wake Mtwa Mkwawa kwa Mama Sengimba mdogo. Picha zote na Admin.
“Kilonge alipofariki akazikwa katika eneo ambalo sasa ni Kijiji cha Lupembe lwa Senga (maana yake Pembe ya Ng’ombe), ambapo kaburi lake lilikuwa na pembe mbili za tembo, ingawa nasikia pembe zile ziliibwa na tunaambiwa walioiba wote walikufa ukoo mzima. Nasikia serikali ilipeleka pembe nyingine na kuzichimbia ili iwe kumbukumbu,” anasimulia Malugala.
Utawala una mambo yake, wakati mwingine unatumia njia halali na haramu ili kuudumisha. Malugala anasema, Munyigumba, ambaye ni mtoto wa pili wa Mtwa Kilonge, alihisi kwamba angeweza kuukosa uchifu kwa kumhofia kaka yake Ngawonalupembe.
“Kwa hiyo akafanya hila na kumuua kaka yake Ngawonalupembe ili yeye atawale, halafu akamchukua Sekinyaga, mke wa marehemu kaka yake kuwa mkewe, lakini wakati anamchukua, kumbe tayari Sekinyaga alikuwa mjamzito.
“Baada ya mtoto kuzaliwa, ambaye alikuwa wa kiume, Mama Sekinyaga akamwita Malangalila Gamoto, pengine kwa maelekezo ya marehemu Ngawonalupembe mumewe. Kwa hiyo Malangalila siyo mtoto wa Munyigumba, bali wa kaka yake ingawa yeye ndiye aliyemlea,” anaeleza Malugala.
Malugala anasimulia kwamba, ugomvi ulitokea baada ya mama huyo kujifungua ambapo alimwambia Munyigumba kwamba huyu siyo mtoto wake. Hapo Munyigumba akakasirika na kuamua kumfukuza Sekinyaga na mwanawe.
Inaelezwa kwamba, alipomfukuzwa, Sekinyaga akaelekea katika maeneo ya Sadani, lakini baadaye Munyigumba akajirudi kwa kuhisi angepata aibu, hivyo ikabidi amrudishe.
“Sasa wafuasi wake aliowatuma wakamchukue huyo mama wakaenda kumuua huko Sadani, hata kaburi lake halijulikani liliko. Wao wakarudi na mtoto Malangalila Gamoto. Kwa hiyo, Malangalila na Mkwawa ni mtu na mdogo wake kasoro baba zao,” anaeleza.
Munyigumba alikuwa na wake watano – Sengimba, Sendale, Sekinyaga (aliyekuwa mke wa kaka yake), Sembame na Sengimba mdogo. Sengimba mkubwa aliwazaa Kilemaganga, Mkwawa, Mpangile, Mulimbila na Wiyolitwe; Sendale alimzaa Mgungihaka; Sengimba mdogo alimzaa Msengele Kilekamagala; Sekinyaga alimzaa Malangalila Gamoto (kwa Ngawonalupembe); na Sembame alimzaa Mpugumoto.

USHUHUDA WA MWAKASEGE UNAGUSA SANA

Mwalimu Christopher Mwakasege
 Mwalimu Christopher Mwakasege alitoa ushuhuda huo katika semina iliyokuwa ikifanyika katika viwanja vya Furahisha jijini Mwanza Semina hiyo iliyokuwa  somo linaloitwa namna ambavyo Roho Mtakatifu awezavyo kukusaidia ili upokee kile unachokiomba.

Alisema Roho mtakatifu akwambiavyo omba hiyo haina MJADALA ni kuingia kwenye maombi mpaka upate unachokiomba kwa kuwa gharama ya kuingia kwenye maombi ili kupata ulichotakiwa kukipata ni ndogo kuliko gharama ya kukosa kile ulichoambiwa ukipate katika Maombi hayo.

Roho mtakatifu anapokupa mzigo wa kuombea jambo anakupa na muda ukizembea muda huo ukipita kinakuwa ni kiporo, na kiporo kinaweza kikalika na kipo ambacho hakiliki.  “Tulipoenda Israel na Fanuel Sedekia kisha akaanza kuumwa madaktari waliniambia ubongo wake kwa asilimia tisini haufanyi kazi. Lakini walishangaa kwa nini kila mara niko pale Hospitali wakasema kwa nini usikae tu Hotelini kisha ukawa unapiga simu kuulizia hali ya Mgonjwa? Wao hawakujua kwa nini naenda pale kwa kuwa suala la kupiga simu tu sio tatizo ningeweza kurudi Arusha kisha nikawa napiga simu.

Suala hapa ni kuwa nilikuwa naenda kila mara kwa ajili ya kumfanyia maombi, nilikuwa nakaa kandokando ya Bahari ya Galilaya nafanya maombi juu ya Sedikia kwa masaa sita nikitoka hapo nasikia upako wa ajabu sana kIsha napanda Taxi kuelekea
Hospitali. Nikifika Hospitali madactari na watu wa ICU walikuwa washanifahamu hivyo naenda moja kwa moja kwenye chumba cha nguo nabadili nguo kIsha naingia ICU alikolazwa.

Nikifika nambana Mungu kwa maswali Mengi namuuliza Sedekia, hivi unaongea nini na Yesu muda wote huo si urudi? na kisha namuuliza Yesu, hivi Yesu si unafahamu kuwa Sedekia anamke
ukimchukua mkewe atamuachia nani? Kisha baada ya maneno hayo naweka mkono juu yake.

Nilipokuwa nikiweka mkono juu yake ghafla upako wote unakuwa kama umenyonywa. Baada ya hapo narudi hotelini naanza tena
kumuuliza Mungu hivi Mungu kama basi husikii maombi yangu sikia maombi ya watanzania kwa kuwa saa hiyo nilijua watanzania wengi wanamuombea Sedekia.
Inafikia wakati nakata tamaa lakini ndani yangu najisemea Mwakasege haiwezekani jitie moyo kisha nabadili aina ya maombi, kwa kuwa nilikuwa na nguo zake pamoja na passport yake nikawa naviweka kati kisha nikawa naanza maombi ya Yeriko, nikawa niko hotelini usiku nazunguka nguo zake na paspot yake huku nikifanya maombi.

Taratibu Mungu akaanza kuniambia kuwa sedekia harudi, Kipidi hicho mimi na familia yangu tulikuwa tumepanga kwenda kupumzika nchini Uingereza wakati wa skukuu ya Chrismass, na booking mpaka ya Hotel tulikuwa tumeshafanya, na watoto wote wako nyumbani wakijiuliza tunaendaje kupumzika wakati Sedekia anaumwa? Chrismass ikapita na mwaka mpya pia kisha Sedekia akafariki.
Baada ya kifo hicho sikuchoka nkarudi tena kwa Mungu nikamuuliza kwa nini Mungu umeamua kumchukua Sedekia mikononi mwangu? Mungu alinijibu vitu ambavyo siwezi kuvisema hapa.

Kila siku mimi ni mgeni katika maombi namhitaji ROHO anifundishe kwa upya kwa kuwa sijui vita gani ninakwenda kupambana nayo, Mungu anabaki kuwa Mungu kwa kuwa hufanya atakavyo”
Ushuhuda huu umeandikwa kwenye facebook na Francisco. Unaweza kumfuatilia kwenye facebook hapa
---------------------------------------------------------------------------------
Kama una ushuhuda na ungetamani tuwashirikishe na wengine kupitia blogu yako ya Kikristo isiyofungamana na dhehebu lolote usiache kuwasiliana nasi kwenye facebook au tutumie kupitia ushuhudainjili@gmail.com

Mungu akubariki sana kwa kufuatana nasi.
Usiache kutufuatilia kwenye Facebook pamoja na Twitter

Tuesday, November 12, 2013


Kitunguu dawa tosha kwa wanaotokwa na damu kwa njia ya haja kubwa

 

 


Katika makala ya leo nawaeleza faida za juisi ya kitunguu maji katika mwili wako, ikiwemo uwezo wake wa kuzuia na kutibu magonjwa sugu na yaliyoshindikana kwa kutumia dawa za hospitali.

Tunapaswa kutambua kwamba viungo vingi tunavyotumia jikoni kwenye vyakula vyetu kila siku vina uwezo mkubwa wa kuponya magonjwa yanayotusumbua. Sina shaka kama kuna mtu ambaye hakijui kitunguu, nyanya, au kitunguu saumu.

Kitunguu maji ni kiungo cha mboga, ambacho aghalabu hutumika katika mapishi ili kuongeza ladha katika chakula na wakati mwingine hutumika kutengenezea kachumbari. Baadhi ya watu hawapendi kula kachumbari kwa kutokujua umuhimu wake mwilini.

KITUNGUU KINATIBU YAFUATAYO
Katika orodha ndefu ya magonjwa yanayotibika PASIPO SHAKA kwa kutumia juisi ya kitunguu, ni pamoja na ugonjwa unaowasumbua watu wengi wa kutokwa na damu sehemu ya haja kubwa wakati wa kujisadidia.

Ugonjwa huu, ambao kwa kitaalamu unajulikana kama ‘hemorrhoids’ au ‘Piles’, unawatokea watu wengi ambao kama mtu hukupata nafuu kwa kula vidonge, suluhisho la mwisho huwa ni kufanyiwa upasuaji mdogo katika njia ya haja kubwa, upasuaji ambao huambatana na maumivu makali.

Kwa wale ambao wameshakutwa na tatizo hili au wanalo hadi sasa, dawa kama vile ANUL SUPPOSITORIES, SECNIDAZOLE, n.k zinajulikana sana kwao, kwa sababu ndiyo dawa zinazopendekezwa na madaktari wengi kutumiwa ili kutibu PILES. Unaweza ukapona kwa muda na tatizo likajirudia baadaye au unaweza usipone na ukalazimika kufanyiwa upasuaji.

Lakini kwa kutumia juisi ya kitunguu, unaweza ukapona kabisa na inawezekana tatizo lisijirudie, kwani mzizi wa tatizo huondoka kabisa kutoka tumboni.

SIFA YA KITUNGUU
Kitunguu kina virutubisho vyenye uwezo wa kuua bakteria (antibacterial) na fangasi mwilini. (anti fungus). Pia kina virutubisho vyenye uwezo wa kuzuia wadudu wanaosababisha magonjwa nyemelezi (anti free radicals) na magonjwa ya uvimbe (anti informatory).

Mbali na sifa hizo, kitunguu kina kiwango kikubwa cha madini kama vile ‘calcium’, ‘magnesium’, ‘sodium’, ‘potassium’, ‘selenium’, ‘phosphorus’ na bila kusahauu kiasi kidogo cha aina fulani ya mafuta ambayo huimarisha kinga ya mwili.
JINSI YA KUJITIBU ‘HEMORRHOIDS.’

Kama nilivyoanza kusema awali, pamoja na magonjwa mengine yanayotibika kwa kitunguu, leo tutaanza kwanza na ugonjwa huu unaosumbua watu wengi. Dawa hii ni ya uhakika kwa mtu atakayeweza kuitumia kama inavyotakiwa.

Kunywa juisi ya kitunguu kila siku asubuhi kwa muda wa siku saba hadi siku 14, ikitegemea na ukubwa wa tatizo lako. Juisi hiyo lazima uinywe asubuhi kabla ya kula kitu chochote (on empty stomach) na utaruhusiwa kunywa kifungua kinywa chako saa moja baada ya kunywa juisi hiyo.

Dozi hii ni maalum kwa ajili ya kutibu ‘hemorrhoids’, ingawa wakati ukitibu tatizo hilo, matatizo mengine yaliyomo mwilini yatakuwa yakijiondoa, kama tutakavyoona katika makala haya wiki ijayo. Napenda kukuhakikishia kuwa tiba hii ni ya uhakika na haina madhara yoyote.

TAHADHARI
Mara baada ya kuinywa juisi hii kwa mara ya kwanza na siku chache zitakazofuata, utajisikia vibaya na tumbo kuchafuka. Hali hii ni ya kawaida, unachotakiwa kufanya mara baada ya kunywa, ni kukaa au kulala kwa muda, baada ya muda hali yako itarejea kama kawaida. Baada ya siku tatu, ukinywa mwili utaizoea na utajisikia kawaida tu.

MSIBA MKUBWA TANZANIA DR MVUNGI AFARIKI DUNIA

Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dkt. Edmund Mvungi (katikati) akibadilishana mawazo na Makamishina wa Tume ya Pamoja ya Fedha (JFC), Dkt. Juma Ngasongwa (kulia) na Mhe. Othman Masoud, ambaye ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) mara baada ya JFC kuwasilisha maoni yao kuhusu Katiba Mpya wakati wa mkutano wao uliofanyika katika viwanja vya Karimjee Jijini Dar es Salaam.

Mvungi Wafanyakazi -
Jumatano Januari 9, 2013: Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk. Edmund Mvungi (katikati) akizungumza na Viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Nchini (TUCTA) waliofika katika Ofisi za Makao Makuu ya Tume Jijini Dar es Salaam leo kuwasilisha maoni yao kuhusu Katiba Mpya.

Na Mwandishi Wetu
Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba aliyekuwa akipatiwa matibabu nchini Afrika Kusini amefariki dunia leo..

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Bw. Assaa Rashid leo jioni (Jumanne, Novemba 12, 2013), Dkt. Sendongo Mvungi majira ya saa 8:30 mchana kwa saa za Afrika ya Kusini akiwa katika Hospitali ya Milpark.

“Kwa masikitiko makubwa, Tume inawafahamisha wananchi kuwa Mjumbe wake, Dkt. Sengondo Mvungi aliyekuwa akipata matibabu katika Hospital ya Milpark iliyopo jijini Johannesburg nchini Afrika Kusini amefariki dunia leo (Jumanne, Novemba 12, 2013) saa 8:30 mchana kwa saa za Afrika ya Kusini,” amesema Bw. Rashid katika taarifa yake fupi ya awali na kuongeza:

“Taratibu za kuusafirisha mwili wa marehemu kutoka nchini Afrika Kusini kuja nchini kwa mazishi zinaendelea na taarifa zaidi zitatolewa kesho (Jumatano, Novemba 13, 2013),” ameongeza.
 

Marehemu Dkt. Mvungi alisafirishwa siku ya Alhamisi, Novemba 7, 2013 kwenda nchini Afrika Kusini kwa uchunguzi na matibabu zaidi akitokea Kitengo cha Mifupa Muhimbili (MOI) aliokuwa amelazwa baada ya kuvamiwa nyumbani kwake Kibamba, wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam na watu waliomjeruhi vibaya kichwani usiku wa kuamkia siku ya Jumapili, Novemba 3, 2013.

Katika taarifa yake, Tume pia imewaomba watanzania wote kuungana na familia, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu Dkt. Mvungi katika kuomboleza msiba huo.

Na Omega S. Ngole
Principal Information Officer,
Constitutional Review Commission (Tanzania),
PO Box 1681,
Dar es Salaam,
Tel: +255 (0) 22 2133425,
Fax: +255 (0) 22 2133442,
Mobile: +255 (0) 757 500800,
Website: www.katiba.go.tz
Facebook:www.facebook.com/people/Omega-Ngole
Twitter: https://twitter.com/OmegaNgole


Fahamu Utamaduni Mila na Desturi ya Mtanzania

Watanzania wana simulizi za kusisimua kuhusu asili yao.  Hapo zamani za kale, kutokana na uso wa ardhi kutokuwa mgumu, ardhi ilipasuka na kusababisha Bonde la Ufa ambalo linatanda kuanzia kusini mwa Yemen kupitia nchi za Afrika ya Mashariki ikiwemo Tanzania, hadi Ziwa Nyasa na kugawanyika magharibi kati ya Tanzania na Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo.  Moja ya sehemu mashuhuri sana katika Bonde hilo ikatokea ndiyo chimbuko la binadamu.  Binadamu wa awali anafanana na nyani na kwamba fuvu lake na nyayo ziligunduliwa na familia ya Leakeys hapo mwaka 1959 na 1979.  Ushahidi huu ambao ni matokeo ya uvumbuzi wa elimukale kuhusu binadamu wa kwanza ulipatikana katika Bonde la Olduvai na Laetoli.  Maeneo hayo yalikuwa baadhi ya makazi ya ukoo safu wa kisasa (homo habilis na homo sapiens), wazee wa kitanzania ambao waliweza kufikiri na kutengeneza vifaa vinavyotokana na mawe.  Mabaki muhimu ya vifaa na mifupa vilivyoachwa na aina ya binadamu, vinakadiriwa kuwa na umri wa miaka milioni moja na sabini na tano elfu.  Aidha, ushahidi kamahuo umechimbuliwa kwenye maeneo ya kihistoria huko Isimila katika Nyanda za Juu za Kusini ambako vifaa vya kale, vijulikanavyo kama shoka vinaweza kuonekana leo.  Michoro kwenye mapango ya Kondoa-Irangi iliyochorwa na babu zetu hao na dalili za shughuli za uhunzi na umwagiliaji maji mashamba ni ushahidi mwingine wa kuwepo kwa dalili za mtu wa kwanza katika Tanzania kwa wakati wa kale.  Ni vyema kusadiki na kukubali kutoka hapo ni kwamba baadhi ya wazao walitawanyika duniani kote na baadaye kurejea Tanzania kujiunga na dada na kaka zao waliobaki hapa nchini.  Hao sasa walirejea kama wapiganaji wakulima, wachungaji walowezi, wavamizi, wakimbizi, wakoloni, wafanyabiashara, wavumbuzi, wamisionari au watafuta watumwa.  Idadi kubwa ya watu hao ndiyo wanaunda jamii ya watanzania wa leo ikiwa ni pamoja na makabila makubwa (asilimia 99) bila kuwajumuisha makundi madogo kutoka  Ulaya na Asia (asilimia 1).  Kutokana na kukosekana kwa hali ya utulivu kama kawaida na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe katika nchi za jirani hivi sasa na hata hapo zamani, Tanzania imekuwa ni mahala pa makimbilio kwa wahamiaji.  Wakimbizi kutoka makutano ya Benini-Benne Africa magharibi, Bahr el Ghazal nchini Sudan na maeneo ya Shunygwaya nchini Kenya wote walihamia Tanzania kati ya karne ya tatu na kumi na tatu.  Hii leo Tanzania bado anapokea na kuwahudumia maelfu ya wakimbizi kutoka Burundi, Rwanda, Somalia na Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo.  Hali hii inaleta mgongano mkubwa kwa idadi ya watu nchini, rasilimali na mazingira.  Idadi ya wakimbizi hao inakadiriwa kuwa kati ya 500,000 hadi 1,000,000.  Wakimbizi wamesababisha athari kubwa kwa nchi hii.  Kutokana na mahitaji ya chakula, maji na kuni, karibu vyanzo vyote vya maji na mimea ya asili ya sehemu husika na jirani ya kambi hizo za wakimbizi zimeharibiwa.  Matokeo yake ni  kwamba maeneo hayo yamegeuzwa kuwa maeneo yasiyokuwa na kitu, maeneo yaliyo katika hali ya jangwa.
 
Mauaji, wizi  na aina nyingine za maovu yamefanywa na baadhi ya wakimbizi na hivyo kusababisha usumbufu kwa jamii na kutoweka kwa amani kwa baadhi ya raia wa Tanzania.  serikali ya Tanzania, Umoja wa Nchi za Afrika (OAU), Shirika la Umoja wa Mataifa la kushughulikia  wakimbizi (UNHCR) na Shirika la Umoja wa Mataifa la Watoto (UNICEF) wanajitahidi kuwarekebisha wakimbizi hao ili wakati muafaka ukifika warejeshwe makwao.
 
Kwa jumuiya ya kimataifa suala la wakimbizi ni eneo lingine ambalo linahitaji msaada zaidi kwa Tanzania ili kuiwezesha kuwasaidia wakimbizi hao kuishi kama binadamu wengine pamoja na kusaidia kuleta amani kwenye nchi zao ili ziweze kuwa mahala pa kuishi.
 

Utamaduni, mila na desturi

Hali ya mvuto wa mfumo ya jamii wa Tanzania ni kivutio kikubwa kwa masuala ya utamaduni, uchumi na utalii.  Hadithi za watu wa kale, ngoma za asilia na aina ya ngoma zinatofautiana kati ya kabila na kabila.  Wanapocheza, Wamakonde kuchezesha viuno vyao kwenda sambamba na ngoma ya “sindimba”, Wazaramo humezwa na maandamano ya “mdundiko”.  Wamaasai huruka kwa mpangilio maalum huko wakitoa  sauti nzito ambazo zinaweza kumwogofya simba dume!  Matumizi ya nyoka hai na kucheza na nyoka wakubwa kama chatu kunakofanywa na Wasukuma wakati wanacheza ngoma ya “Bugobogobo” hakuwezi kusahaulika kwa mgeni.  Kila kabila kati ya  makabila 120 ya Tanzania ina ngoma yake na staili zake za uchezaji ambazo zinapumbaza kwa kukazia macho zinafurahisha na kuvutia kijinsia.
 
Aina mbalimbali ya mavazi pia hutoa mvuto  wa aina yake kwa mgeni.  Wanaume wa Kimasai huvaa vazi ambalo halifuniki mwili wote huku wakitembea na mikuki, virungu na visu vikubwa.  Kwa upande wao, wanawake wa Kimasai hujaza tele shingo zao, mikono, miguu na masikio yao na vitu vya thamani vikiwemo shanga na hadi aina nyingine za madini.  Wanaume wa Kimasai hupakaza miili yao na udongo mwekundu uliochanganywa na mafuta yatokanayo na wanyama na husuka nywele zao.

Wamakonde nao huchonga meno yao na kuchanja nyuso na miili yao taaluma inayotamanisha.  Wamakonde ni wataalam wa kuchonga vinyago vinavyoonyesha matatizo ya binadamu, mapambano, mapenzi, tamaa, wema, ubaya na mshikamano vitu ambavyo vinavutia sana na kuamsha fikra.
 
Wakazi wa pwani na visiwani hupamba mikono, miguu, midomo na kucha kufuatana na tukio shughuli ambayo huleta mvuto mkubwa.
 
Kati ya makabila ya namna ya pekee ni makundi ambayo yanakadiria kutoweka yaishiyo kati ya Tanzania.  Makabila  haya ni ya Wasandawe (wanahusiana na Waethopia) ambao jirani zao ni wa Iraqw gorowa na burungi na Wadzapi ambao pia hujulikana kama Watindiga na Wakangeju na Wahontetot - wanaohusiana na kabila la Khosa la Afrika Kusini ambao huzungumza lugha za “click”.  Wandorobo pia wanazungumza lugha hiyo lakini wameiga zaidi utamaduni wa nje ya mazingira yao.  Watanzania hao ni wa kuhamahama, wachumaji matunda, wawindaji wakusanyaji chakula, na wavuvi waishio katika eneo linalozunguka Ziwa Eyasi ambalo liko kilomita chache kutoka bonde maarufu la Ngorongoro.  Inasemekana kwamba idadi ya watu hawa kwa sasa haifikii 500 wakati mwaka 1965 walikuwa zaidi ya 30,000.

Wito hapa ni kuisaidia Serikali ya Tanzania kuwaokoa watu hao wasifikie ukingo wa kutoweka.  Kwa maana hiyo, maeneo yanayozunguka Ziwa Eyasi ni bora kabisa ya kufanyia utafiti wa kisayansi wa elimu ihusuyo habari za asili na maendeleo ya  binadamu kwa ajili ya kumbukumbu za baadaye.  Kinachojitokeza ni kwamba ni vyema kutambua kuwa huu ni wakati muafaka wa kufanya uchunguzi ama vile watu hao watakuwa wametoweka kabisa.