JE WAJUA MKWAWA ALIVYOWATEKETEZA WAJERUMANI KWA DAKIKA 15 TU!!!
HUU ni mfululizo wa Makala ya Uchunguzi kuhusiana na historia ya
kiongozi mkuu wa Wahehe, Chifu Mkwavinyika Munyigumba Kilonge
Mwamuyinga, maarufu kama Mkwawa, kama yanavyoandikwa na Mwandishi Wetu, ambaye amefanya uchunguzi kwa takriban miezi mitatu sasa
katika kuhimiza utalii wa ndani na kuhifadhi historia yetu. Endelea na
Sehemu hii
HADI wakati huo, tayari von Heydebreck – mmoja wa manusura katika
vita hivyo – alikuwa amekwishajeruhiwa na kuanguka akiwa amepoteza
fahamu, lakini baadaye aliandika kwenye ripoti yake
“…Mfululizo wa
matukio hadi wakati huu ulikuwa umetumia dakika mbili au tatu tu.
Nilitambua hilo kabla ya kujeruhiwa, Wasudani tayari walikuwa wamekimbia
kurudi nyuma vichakani baada ya kufyatua risasi mara mbili hivi. Mimi
na askari wa Kikosi cha Tano tulilazimika kujilinda na kujitetea baada
ya kuona Wahehe wakija katika umbali wa hatua 30. Kama sikosei, nilimsikia
Sajini Tiedemann akisema alikuwa ameumia kabla hajafyatua risasi.
Haikuwa rahisi kuona zaidi ya umbali wa hatua tano msituni kutoka pale
njiani. Pia hakuna ambaye aliweza kunusurika kwa sababu Wahehe walikuja
kwa kasi… Ni wazi walipanga kutushambulia baada ya kufika katikati
msitu. Kuvurugika kwa mipango yao kulichangiwa hasa na kitendo cha
Luteni von Zitewitz kufyatua risasi…”
Muanzilishi wa Himaya ya Ujerumani Afrika Mashariki, Carl Peters,
baadaye Novemba 23, 1891 alimwandikia Gavana von Soden akisema kwamba,
katika mapambano mengine na makabila mbalimbali ya Tanganyika, ilikuwa
ni bahati tu kwao kutoweza kupata madhara kama waliyopata Wajerumani
pale Lugalo, kwani mafunzo yao ya vita yalikuwa yanalenga zaidi kupigana
wakiwa wamejipanga pamoja kwa mbinu maalum. Hawakuwa wamejifunza
kupigana kila mtu kwa uwezo wake, bali walitegemea zaidi kushambulia kwa
pamoja.
Iliwachukua Wahehe dakika 15 tu (kuanzia saa 1:15 hadi 1:30 asubuhi)
kuwafyeka Wajerumani na majeshi yao. Von Zelewiski aliuawa kwa kupigwa
nyundo kichwani akiwa amepanda punda wake wakati akijiandaa kuwafyatulia
risasi wapiganaji wa Mkwawa. Kabla hajadondoka akachomwa mkuki ubavuni.
Hii ndiyo asili hasa ya jina la ‘Nyundo’ kutokana na kamanda huyo wa Wajerumani kuuawa kwa nyundo!
Kuhusiana na kifo cha Kamanda von Zelewiski, kama Mjerumani Tom von
Prince alivyoandika baadaye, “Kama nilivyosimuliwa baadaye… na Wahehe
walioshuhudia, alijitetea mwenyewe kwa kutumia bastola yake kubwa na
kuwapiga risasi watu watatu, wakati kijana mmoja wa Kkihehe alipomchoma
na mkuki ubavuni. Kijana huyo alikuwa na umri wa miaka 16 tu na
alizawadiwa ng’ombe watatu na Mkwawa kwa kitendo hicho.”
Luteni von Pirch na Dk. Buschow pia waliuawa wakiwa juu wa punda wao
ambapo majeraha yao yalikuwa makubwa mno. Karibu askari wote wa Kikosi
cha 7, Kikosi cha Silaha, Kikosi cha 5 na baadhi ya askari wa Kikosi cha
6 waliuawa kabla hata hawajajua wafanye nini.
Luteni von Heydebreck, Luteni Usu Wutzer na Murgan Effendi pamoja na
askari 20 hivi ndio waliofanikiwa kukimbia kutoka eneo hilo la mapigano
na kukimbilia upande mwingine wa mlima na kuweka ngome wakijilinda dhidi
ya mashambulizi ya Wahehe. Wapiganaji hao wa wajerumani walijificha
kwenye pagala moja la tembe lililokuwa limetelekezwa mlimani. Askari
mmoja Msudani ndiye aliyekiona kibanda hicho.
Lakini von Heydebreck aliishuhudia vita hiyo katika kipindi cha
dakika mbili au tatu tu kabla ya kupoteza fahamu. “Kulingana na ushuhuda
wa Wahehe walioshiriki mapigano yale, vita hivyo havikumalizika mapema
kama ambavyo Wazungu wa mstari wa nyuma walivyotegemea, badala yake
askari walionusurika waliendelea kupambana hadi saa 4:30 asubuhi na
kuwaua maadui wengi (Wahehe).”
Askari wa mwisho wa kikosi cha Luteni von Tettenborn ndio hawakupata
madhara makubwa ya mashambulizi ya Wahehe, washukuru kutokana na makosa
ya ishara, vinginevyo wote wangeangamia katika kipindi hicho cha dakika
15 tu. Von Tettenborn, Feldwebel Kay na askari kama 20 hivi Wasudani
wakahamia upande wa kushoto wa eneo la mapigano na kutengeneza nusu
duara kwa ajili ya mashambulizi huku wakiwa wameumia. Wakiwa hapo
walipandisha bendera ya Ujerumani juu ya mti na kupiga mbinja ili
kuwaita manusura wengine.
Wakati huo Wahehe waliendelea kuwakimbiza manusura na kushambulia
kila waliyemuona mbele yao. Mkanganyiko ukaongezeka baada ya kuwasha
nyasi.
Mnamo saa 2:30 asubuhi hiyo, Luteni von Heydebreck, Luteni Usu Wutzer
na Murgan Effendi wakiwa na askari wao 12 walipenya na kuungana na
kikosi cha von Tettenborn. Von Heydebreck alikuwa anavuja sana damu
kutokana na majeraha mawili makubwa ya mikuki. Kwa kuwatazama tu watu
hao, von Tettenborn akatambua kwamba vikosi vyao vyote vilikuwa
vimesambaratishwa na kikosi cha silaha kutekwa, ambapo Mkwawa aliteka
bunduki 300. Askari wa jeshi la Wajerumani waliouawa siku hiyo walikuwa
zaidi ya 500.
Ilipofika saa 3:00 Luteni Usu Thiedemann, akiwa na majeraha makubwa
ya moto aliingizwa kwenye kikosi cha Luteni von Tettenborn akiwa
amebebwa na askari waliokuwa wanafanya doria. Nyasi zilizokuwa zinaungua
sasa zilimtisha von Tettenborn na manusura wengine.
Hadi kufikia saa 10:00 jioni Luteni von Tettenborn alikuwa
amewakusanya majeruhi wengi na kuokota baadhi ya mizigo yao. Wahehe
waliokuwa wamepagawa kwa hasira pamoja na moto mkubwa uliokuwa
ukiendelea kuteketeza msitu viliifanya kazi ya kuwatafuta majeruhi
wengine kuwa ngumu, hivyo wengi waliteketea kwa moto. Von Tettenborn
akaamua kuanza kurudi nyuma kabla hajazuiwa na Wahehe.
Wakati wa usiku wa manane kikosi kilichokuwa na Luteni von Tettenborn
kikapiga kambi ng’ambo ya pili ya mto tofauti na mahali walipolala
kabla ya kuanza mapambano. Kikosi chake sasa kilikuwa na yeye mwenyewe
na Luteni von Heydebreck, ma-NCO watatu wa Kijerumani (ingawa Luteni Usu
Thiedemann alikufa baadaye njiani), maofisa wawili wa Kiafrika, ma-NCO
62 wa Kiafrika, wapagazi 74 na punda 7. Kutoka hapo wakaanza kutembea
hasa nyakati za usiku kurudi nyuma ambapo walifika Myombo Agosti 29.
Hakuna takwimu halisi za idadi ya Wahehe waliokufa kwenye vita hiyo
ingawa makadirio ni kati ya 260 hadi 700. Kwa ujumla, Wajerumani
walikuwa wameshinda vita dhidi ya wakoloni, ushindi ambao ni wa
kihistoria kwa mtawala yeyote wa Kiafrika wakati huo dhidi ya Wazungu.
Haya yalikuwa matokeo mabaya zaidi kwenye vita katika historia ya
ukoloni wa Wajerumani.
Jeshi la Wahehe halikuwa na haja ya kuhitimisha ushindi wake kwa
kuwafuatilia Wajerumani waliosalia ili kuwaangamiza kabisa. Badala yake,
kuanzia wakati huo wakaendelea kuishambulia misafara yote ya Wazungu.