ADVERT 1

ADVERT 1
Kilio na kimbilio la wanahabari Tanzania

Friday, September 28, 2012





BAADHI ya wananchi wamesema utajiri wa Mchungaji Anthony Lusekelo ‘Mzee wa Upako’ (pichani) unatisha.
Hivi karibuni, Lusekelo alisema kuwa mwaka uliopita pekee, alitumia  shilingi milioni 380, kulipia vipindi vya runinga ili kuwafikia Watanzania.
Kutokana na hilo, wananchi wameliambia Uwazi kuwa Lusekelo ni tajiri mkubwa kutokana na kauli yake mwenyewe kwamba anatumia mamilioni kuendesha vipindi vya runinga.
Akizungumza mwishoni mwa wiki iliyopita katika moja ya vipindi vyake, Lusekelo alisema fedha hizo zimemuwezesha kutoa neno kwa Watanzania wengi kupitia televisheni.
“Niwashukuru wote waliochangia kipindi cha Tutashinda. Hiki ni kipindi changu. Kuna wengine wanasema kwa nini jina la akaunti ni langu, nasema hiki ni kipindi changu na hizi fedha ni zangu siyo za kanisa,” alisema Mzee wa Upako.
Aliongeza kuwa hata akifa kipindi hicho kitakufa kwa kuwa ni chake lakini akasema Mungu huwa anaweka mbadala pindi anapoona anataka kumuondoa  mtumishi wake duniani.
Mchungaji huyo wa Kanisa la GRC alisema, anawashukuru waumini wote wanaolichangia kanisa kwani awali lilijengwa likiwa na uwezo wa kuchukua watu 70 tu lakini sasa linabeba watu 5,000.
“Nilianza kazi hii ya kuhubiri neno la Mungu Iringa Stendi mwaka 1983. Nina miaka 29 katika kazi hii, japokuwa ukiniangalia utafikiri mimi bado ni kijana, nasema tushukuru na kujivunia hili.
“Samahani kwa kusema haya kuwa Kanisa la KKKT (Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania) lilianzishwa na Martin Luther King na linapewa ruzuku na serikali ya Ujerumani lakini GRC halisaidiwi na serikali, ni nguvu ya waumini, nawapongeza sana,” alisema Lusekelo.
Inasekana kuwa Lusekelo amefunguliwa na Mungu kwa kupewa uwezo wa kuombea watu na alianza kazi ya utumishi huo akiwa katika hali ya chini, akihutubia kwa kutembea kwa miguu mitaani lakini hivi sasa anatumia gari aina ya Range Rover Sport.
Inaelezwa kuwa wengi  wanaamini huduma yake, ndiyo maana wakiambiwa wamchangie, huwa hawasiti, hivyo kumuwezesha kupata utajiri anaoutumia kuwafikia waumini.

TATIZO HILI LA KAZAGAA KWA TAKA IRINGA VIONGOZI MNAONA? AU BADO MPO MPO KWANZA?

(Story kwa hisani ya Francisgodwin.blogspot.com) 
 
hapa ni kata ya kweakilosa eneo la kota za polisi taka zikiwa zimejazana barabarani
Hizi ni takataka zilizojaachwa bila kutolewa katika kata ya Ilala kata anayotoka naibu meya wa Manispaa ya Iringa Grevas Ndaki
uchafu huu ukiwa umezagaa kota za polisi Frelimo baada ya Manispaa ya Iringa kushindwa kutoa taka zilizomwangwa na wananchi katika kituo cha taka eneo hilo
Hapa ni Ilala taka zikiwa zimemwangwa nje ya nyumba ya mtu.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa Teresia Mahongo
Mwandishi wa makala  haya Bw Fredrick Jailos anaanza kwa  kuhoji  kuwa , Tumekosea Wapi?Tatizo la kuzagaa kwa taka taka katika Manispaa ya Iringa mkoa wetu wa Iringa linakua kwa kasi kila siku.
hili licha ya kua linaharibu sifa na hadhi ya mkoa wetu kama moja ya mikoa misafi Tanzania, pia linahatarisha maisha ya viumbe hai - binadamu, mimea, wanyama na viumbe vidogo kabisa (micro-organisms) Sifa ya usafi kwa mkoa wa Iringa imedumu kwa miaka kadhaa, lakini kwa hali ilivyo sasa, yawezekana sifa hiyo ikapotea.
Miaka kadhaa iliyopita, Iringa kulikua na makontena makubwa kwa ajili ya kuhifadhia taka katika mitaa. Baada ya siku mbili tatu, gari lilipita kubeba makontena hayo na kwenda kumwaga uchafu katika dampo la manispaa.
kontena lilirudishwa sehemu ile ile na wananchi wakaendelea kulitumia kuhifadhi taka! Tatizo la kuzagaa kwa uchafu katika mitaa mbalimbali ya mkoa wa Iringa kwa kiasi kikubwa lilipungua, na mji kuonekana msafi kwa muda mwingi.
Zaidi ya makontena hayo, kuna baadhi ya mitaa ilijengewa vizimba kwa ajili ya kuhifadhi takataka.Vizimba hivyo viliwezesha uchafu wa aina tofauti kuhifadhiwa hapo mpaka siku ambayo gari itapita na kuukusanya.
 Kwa hali ya sasa, vizimba hivyo vimekua vikiachwa kwa muda mrefu bila kuondolewa takataka zilizorundikana ndani yake hivyo kusababisha usumbufu kwa jamii zinazoishi karibu kabisa na vizimba kwani uchafu huo hutoa harufu na kusambaa eneo lote la makazi
. Unapopita katika mitaa ya Iringa leo hii, utakuta hali tofauti! Makontena mengi hayapo kwenye maeneo yaliyokuwepo na kusababisha wananchi kutupa taka chini! Makontena ambayo yamebaki katika baadhi ya maeneo hayatolewi mara kwa mara kwa ajili ya kwenda kumwagwa uchafu kama ilivyokua zamani.
 Hali hii inasababisha makontena hayo kujaa kupita kiasi, mpaka inafikia hatua wananchi wanamwaga taka taka chini. Takataka hizo hukaa hapo kwa muda mrefu mpaka kuja kutolewa.
Uwepo wa takataka hizo sehemu moja kwa muda mrefu husababisha harufu mbaya katika eneo husika, na harufu hiyo husafiri mpaka kufikia umbali wa mita 200 kutoka sehemu yenye uchafu.
Taka taka za plastiki, karatasi na chupa pia zinasafirishwa na upepo, maji yanayotembea, na shughuli za binadamu kufikia mpaka umbali wa zaidi ya mita 500 na kwenda kuchafua mazingira ya mitaa au maeneo mengine.
Ingawa kwa kiasi kidogo, lakini kuna taka za sumu (kemikali) zinazotupwa katika vizimba na makontena yaliyoko sehemu za makazi (mf. Makopo ya kemikali zinazotumika katika saluni za kiume na za kike).
Taka taka za namna hii zikikutana na jua na maji husababisha mmenyuko wa kemikali (chemical reaction), na kupelekea uharibifu wa mazingira! Pia, takataka za kemikali zinaweza kusafiri umbali mrefu ndani/chini ya ardhi na kusababisha eneo kubwa kuathirika. Tatizo hili yawezekana linasababishwa na mambo yafuatayo:
I. Ukosefu wa sheria ndogo ndogo zinazosimamiwa vizuri katika suala la uhifadhi wa taka.
II. Upungufu wa mapipa madogo ya kuhifadhia takataka katika mitaa mbalimbali ya mkoa wa Iringa.
III. Ongezeko la idadi ya watu wanaoishi ndani ya manispaa – hii imesababisha kuongezeka kwa matumizi ya vitu/vifaa mbalimbali na kuongeza wingi wa taka taka zinazozalishwa kwa siku.
IV. Kuchakaa kwa baadhi ya makontena ya kuhifadhia uchafu, pia kubomoka kwa vizimba. Hii imesababisha upungufu wa vifaa hivyo, na kuwalazimu wananchi katika baadhi ya mitaa kumwaga taka taka chini.
V. Ukosefu wa elimu ya mazingira kwa wananchi wa kawaida na kupelekea matumizi mabaya ya vizimba na makontena ya kuhifadhia taka.
VI. Kutokua na utaratibu na usimamizi mzuri wa vizimba na makontena ya kuhifadhia uchafu.
\VII. Ratiba ya gari ya kuzoa taka haiko
wazi na haieleweki. Pia, kuna upungufu wa magari ya kufanya kazi hii.
VIII. Uzembe wa baadhi ya watendaji wa manispaa katika kusimamia suala la udhibiti wa taka.
NI NIN ATHARI ZA TAKATAKA HIZI. a. Uharibifu na Uchafuzi wa Mazingira. b. Kusababisha magonjwa ya mlipuko. c. Kuharibu sifa na mandhari ya mji. d. Kupunguza uwezo wa uzalishaji wa ardhi (rutuba) e. Kuchochea ukuaji au mazalia ya vimelea vya magonjwa kwa wanyama na mimea mingine.
NINI KIFANYIKE? Kiujumla, suala la uhifadhi na usimamizi wa taka ni suala linalohitaji pesa na maandalizi ya kutosha. Lakini kuna ulazima wa suala hili kupewa uzito unaostahili ili Iringa, wananchi wake na viumbe wengine waendelee kuwa salama. Baadhi ya mambo yanayoweza kusaidia kupunguza tatizo hili ni pamoja na;
 i. Kuwe na sheria ndogo zinazosimamiwa vizuri za uhifadhi wa taka katika maeneo ya mjini. Sheria hizo zaweza kuwa sawa au zinazofanana na zile zinazotumiwa katika mkoa wa Kilimanjaro katika uhifadhi wa taka (Kwa Mkoa wa Kilimanjaro, ni marufuku kutupa taka taka hovyo, na hilo linazingatiwa na wananchi kwani kuna usimamizi mzuri wa sharia hiyo ndogo)
 ii. Kuna haja ya kutafuta makontena zaidi na kuyaweka katika maeneo mengi zaidi. Kutokana na kuongezeka kwa kasi kwa idadi ya watu mkoani Iringa (kukichangiwa na uwepo wa vyuo vikuu vitatu), kuna haja ya kuongeza idadi ya vizimba na makontena katika kila mtaa wa manispaa yetu.
 iii. Elimu ya uhifadhi wa taka itolewe kwa wananchi wa kawaida. Serikali ya mkoa kwa kushirikiana na wadau wengine wa mazingira mkoani Iringa (na kwingine) iandae mafunzo ya elimu ya uhifadhi wa taka kwa ngazi ya kata na mitaa (wenyeviti, watendaji, mabalozi nk.). Elimu hii inaweza kutolewa kwa viongozi wa kata na mitaa. Viongozi hao wawajibike kuifikisha elimu hii kwa wananchi wa sehemu zao.
 iv. Ushirikishwaji wa wadau wa mazingira katika program ndogo ndogo ni muhimu. Kwa Mfano EBONY FM wamewahi kuwa na shughuli za kuchangisha pesa kwa ajili ya kununua mapipa ya takataka kwa ajili ya mitaa ya Iringa mjini. Wadau zaidi wakipewa mwamko, kutakuwa na unafuu kwa kiasi kikukwa.
v. Ratiba ya gari ya kubeba taka iwekwe wazi kwa viongozi wa kata/mitaa ili kupunguza tatizo la vizimba na makontena kujaa kupita kiasi.Kuwepo na ratiba ya wazi kwa wananchi kuhusu siku za kukusanya takataka kwenye mitaa. Kwa kila kizimba au mtaa, ziwepo siku maalumu za kukusanya taka, na wananchi wa maeneo husika waambiwe siku hizo. Kwa kufanya hiyo itasaidia katika kutoa taarifa pale gari ya kutoa takataka itakaposhindwa kufika katika mtaa. Pia, inaweza kusaidia kwa wananchi kujipangia utaratibu wa kupeleka taka katika vizimba na makontena.
 vi. Kuna haja ya kuongeza gari za kuzolea taka ndani ya manispaa. Hii inaweza kufanyika kwa manispaa kununua gari zaidi, au kutoa zabuni kwa makampuni binafsi kwa ajili ya kazi hii.
vii. Kuna haja ya kuwa na mafunzo ya uhifadhi wa mazingira mashuleni. Zaidi ya mitaala ya elimu inayozungumzia uhifadhi na usimamizi wa mazingira, manispaa (kupitia idara au kitendo kinachojihusisha na usimamizi na uhifadhi wa mazingira) wanaweza kuandaa program maalum ya kupita mashuleni na kutoa elimu na mafunzo kuhusu uhifadhi wa taka. Kwa njia hii, kaya nyingi za mitaa mingi zitafikiwa kiurahisi. Program hii ihusishe shule za misingi na sekondari.
viii. Manispaa iwe na mtu/watu maalumu, ambaye ni mtaalamu wa mazingira kwa ajili ya kuratibu na kusimamia shughuli za uhifadhi wa taka tu. Mtu huyo anaweza kutoka katika kitengo cha mazingira au kuajiliwa. Kwa kuwa na watu wa namna hiyo, itakuwa ni rahisi kufahamu hali ya mkoa wetu, na pia kuwajibishana pale inapobidi.
ix. Utaratibu wa watu kupita nyumba kwa nyumba kukusanya uchafu mara moja au mbili kwa wiki utasaidia kupunguza tatizo hili. Kila kaya itatakiwa kuhifadhi taka taka zake, mpaka siku ambayo timu itapita kuukusanya na kwenda kuutupa sehemu husika.
Kwa huduma hii, kila familia itatakiwa kulipia kiwango cha pesa kitakachokubaliwa (mf. Tshs 500/ kwa kila familia). Hitimisho Miaka kadhaa iliyopita Iringa ilikuwa inasifika kama mkoa msafi zaidi Tanzania. Lakini kwa sasa hatupo tena kwenye nafasi hiyo.
Na hata kama tunaingia kwenye mikoa mitatu misafi zaidi nchini, hatustahili kuwepo kwenye nafasi hiyo kwani hali yetu ni mbaya(Ingawa walioko nyuma yetu wana hali mbaya zaidi). Tuna vichache vya kujivunia katika suala la uhifadhi wa mazingira, alkini juhudi zaidi zinahitajika ili kuurudisha mkoa kwenye heshima yake ya awali.
 Tuangali tulipokosea na tujisahihishe kabla kipindupindu na magonjwa mengine ya mlipuko hayajatushambulia. Ingawa jukumu hili linaonekana kuwa la uongozi wa manispaa zaidi, lakini wananchi wanahusika kwa kiasi kikubwa kulifanikisha hili.
 Ushirikishwaji wa wananchi na wadau wengine (vyombo vya habari, AZAKI, NK) katika uhifadhi wa taka, kuanzia ngazi ya kaya utasaidia kupunguza tatizo hili kwa kiasi kikubwa. Hivyo basi, kuna haja ya manispaa kujipanga upya katika mpango wake wa uhifadhi wa taka na kutia nguvu zaidi sehemu zenye mapungufu. Tumepotea njia, ytunakoenda ni kule tulipotoka miaka mingi iliyopita.
Hatua inayofuata ni kujipanga upya na kutafuta njia sahihi ya kutufikisha tulipokuwa tunatakiwa kwenda. Mazingira safi na salama ni haki ya kila mmoja wetu. Hivyo ni wajibu wa kila mwana Iringa kuhakikisha kuwa anawajibika kuhifadhi mazingira hayo.
 Na ili wajibu huu uwe sahihi, wananchi wafundishwe/waelekezwe ni nini wanatakiwa kufanya ili tuendelee na safari kuelekea kwenye sifa ya mji wenye mazingira safi na salama zaidi Tanzania.


mkazi wa Frelimo akitoka kutupa taka kata eneo hilo hilo ambalo taka zimezagaa
Kwa  hali  hii  uongozi  wa Manispaa ya Iringa akiwemo  mbunge mchungaji Peter Msigwa na  wabunge  wa viti maalum Ritta kabati  (CCM) na Chiku Abwao (chadema) sasa  wanapaswa  kuendelea  kuimba  wimbo  wa usafi katika mji  wa Iringa .

Haitoshi kwa  viongozi hao  wa kisiasa  pia mkuu  wa mkoa  wa Iringa Dkt Ishengoma na katibu tawala Bi Mpaka  pamoja na mkuu  wa wilaya ya Iringa Dkt Warioba ambao kimsingi ni  wakazi  wa Manispaa ya Iringa hawana sababu ya  kuendelea  kuzichekea  takataka  hizo wanapaswa  kushirikiana na mkurugenzi wa Manispaa ya Iringa na madiwani  wa kata zote  kuzichukia na kuzishughulikia vinginevyo mkoa  wa Iringa utaongoza kwa aibu kwa ajili ya Manispaa ya Iringa .

Tuesday, September 11, 2012

MAREKANI TENA...............................







Kwa mara nyengine tena Marekani imetangaza kuwa inapinga Palestina kuwa mwanachama kamili katika Umoja wa Mataifa.Victoria Nuland, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani amesema Washington inapinga juhudi mpya zinazofanywa na Wapalestina za kutaka Palestina itambulike kuwa nchi huru katika Umoja wa Mataifa. 

Siku chache nyuma, Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina aliwaambia waandishi wa habari huko mjini Ramallah katika Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan kuwa tarehe 27 ya mwezi huu wa Septemba atawasilisha tena ombi la uanachama wa Palestina katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Hivi sasa Palestina ni mwanachama mtazamaji tu katika Umoja wa Mataifa asiye na uwezo wa kupiga kura, na matumaini ya viongozi wa Kipalestina ni kuona wanachama wa umoja huo wanaikubali Palestina kuwa mwanachama rasmi na kamili wa Umoja wa Mataifa.

 Ombi la kutaka kutambuliwa rasmi nchi huru ya Palestina mji mkuu wake ukiwa ni Baitul Muqaddas liliwasilishwa na Mahmoud Abbas kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, lakini halikupasishwa kutokana na uungaji mkono wa kila hali wa Marekani kwa utawala wa Kizayuni wa Israel, pingamizi za Washington ndani ya Umoja wa Mataifa pamoja na msimamo dhaifu wa maafisa wa umoja huo. Hadi sasa karibu nchi 140 zimetangaza kuwa zinaunga mkono mpango wa kuundwa nchi huru ya Palestina. Katika miezi ya hivi karibuni Wapalestina wameanzisha kampeni kubwa kwa lengo la kutaka Palestina itambuliwe kuwa nchi huru na Umoja wa Mataifa, na juhudi hizo za Wapalestina kupigania haki yao hiyo zimepata uungaji mkono mkubwa kimataifa. 

Lakini hayo yanajiri katika hali ambayo katika kuendeleza upinzani wake kwa juhudi hizo za kuhakikisha Wapalestina wanapata haki zao ikiwemo kuunda nchi yao huru, Marekani inaweka vikwazo na pingamizi ili kufelisha na kukwamisha tena juhudi za Wapalestina za kutaka kutangazwa kuundwa nchi huru ya Palestina katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mnamo mwishoni mwa mwezi huu. Marekani ndiyo nchi pekee inayopinga suala hilo, ambapo kwa kutumia kila aina ya mbinu zikiwemo za kutishia kutumia kura yake ya veto dhidi ya ombi la Wapalestina katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa imeviza na kufelisha juhudi za Wapalestina za kutaka Baraza la Usalama lipasishe azimio la kutambuliwa rasmi nchi huru ya Palestina. Vizuizi na pingamizi hizo za Marekani zinakinzana kikamilifu na maazimio yaliyopasishwa na Umoja wa Mataifa ambayo yanaunga mkono na kutilia mkazo haki za Wapalestina kujiamulia mustakabali wao na kuwa na nchi yao huru. 

Kuhusiana na nukta hiyo mwaka 2010 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha kwa wingi mkubwa wa kura azimio la kuunga mkono haki ya taifa la Palestina kujiamulia mustakabali wake. Azimio hilo lilisisitiza na kutilia mkazo kwa mara nyengine tena haki ya wananchi wa Palestina kuamua juu ya mustakabali wao ikiwemo kuwa na nchi yao huru.

 Pamoja na hayo hatua hiyo iliyochukuliwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na uungaji mkono wa nchi nyingi duniani kwa haki za taifa la Palestina umekosolewa na kulaumiwa na Marekani, ambayo ndiyo muungaji mkono mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel, kitendo ambacho kinadhihirisha upeo wa juu kabisa wa uadui wa Washington kwa wananchi madhulumu wa Palestina

UN YAPOKEA HILI..............





Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amekaribisha kuchaguliwa Rais Mpya wa Somalia na kuitaja hatua hiyo kuwa ni kumalizika kipindi cha mpito nchini humo. 

Ban Ki Moon ametoa taarifa kwa mnasaba wa kuchaguliwa Rais Mpya wa Somalia Hassan Sheikh Mahmoud na kueleza kuwa Umoja wa Mataifa unalipongeza bunge jipya la Somalia kutokana na uchaguzi huo kufanyika katika mazingira ya utulivu na ya amani. 

Ban Ki Moon amekaribisha kukamilika mchakato wa kipindi cha mpito huko Somalia na kumtaka Rais Hassan Sheikh Mahmoud kuwa na nafasi kuu katika mchakato wa ujenzi mpya na kurejesha uthabiti huko Somalia kwa kuchagua serikali yenye nguvu. 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa aidha ametaka kuendelezwa mashirikiano na misaada ya nchi jirani na Somalia ili kurejesha uthabiti na usalama